• Nairobi
  • Last Updated December 3rd, 2023 8:00 PM
Mapenzi ya mzazi: Baba akubali kupoteza maisha mwanawe achangiwe pesa kutibiwa figo, wote wakiugua maradhi sawa.

Mapenzi ya mzazi: Baba akubali kupoteza maisha mwanawe achangiwe pesa kutibiwa figo, wote wakiugua maradhi sawa.

NA MERCY KOSKEI

WAAMA wahenga hawakukosea waliponena upendo wa mzazi hauna kipimo wala kikomo.

Stephen Kimani mwenye umri wa miaka 67 amedhihirisha kauli hiyo, baada ya kujitolea mwanawe Zacchaeus Kiarie, 43, achangiwe fedha mwanzo kupata matibabu ya figo, licha ya kuwa mzee huyo anaugua ugonjwa huohuo.

Wawili hao ambao ni wakazi wa Kaunti na Nakuru, walianza kuugua maradhi ya figo wakati tofauti tofauti lakini kwa sasa wanaendelea na matibabu kwa pamoja licha ya gharama ghali.

Kulingana na Bw Kimani, matatizo yake yalianza mwaka wa 2005 alipopatikana na ugonjwa wa Kisukari na kulazwa hospitalini kwa mara ya kwanza maishani mwake.

Anasema kuwa aliendelea na matibabu lakini ugonjwa ulimzidi na kumlazimu kuacha kazi ya ualimu mwaka wa 2004, baada ya hali yake ya afya kudhoofika.

Hata hivyo, miaka 15 baadaye, Bw Kimani alithibitishwa kuugua ugonjwa wa figo na daktari wake alimshauri afanye upandikizaji wa figo (kidney transplant).

Habari hiyo ilimchoma moyo, haswa kutokana na umri wake, akisema kuwa hakuona haja na kumwomba daktari aendelee na matibabu tu.

“Nilimkashifu daktari nikimuuliza ikiwa ananitayarisha kufa. Kutokana na umri wangu niliona itakuwa vigumu kufanyiwa pandikizi la figo. Daktari alinieleza kuwa pia watu wa rika langu wanafanikiwa lakini sikushawishika,” alisema.

Hata hivyo, anabainisha kuwa familia yake ilikuwepo kwa ajili yake hasa Kiarie ambaye alijitwika jukumu la kuhakikisha anapata matibabu bora na kuwa anahudhuria ‘dayalisisi’.

Mnamo Septemba 2022, familia hiyo ilikumbwa tena na janga lingine.

Wakati huu Kiarie aligundulika ana tatizo la figo baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Bw Zacchaeus Kiarie, 43, ambaye anaugua ugonjwa wa figo. PICHA|MERCY KOSEKI

“Nilifahamu hali yangu nilipokuwa nikifanya kazi Murang’a, hatua iliyonifanya nirejee nyumbani na kuanza matibabu. Daktari alishauri nifanyiwe pandikizi la figo, baba akajitolea nichangiwe mwanzo ili niweze kutunza familia yangu jambo ambalo kama familia lilitushtua wengi,” alisema

Kwa sasa Kiarie analazimika kuhudumia dayalisisi pamoja na babake, na anakiri kuwa ni ghali kwani kila kipindi inagharimu Sh 9, 600, kila mmoja.

“Safari yetu imekuwa ya baba na mwana wakienda kufanyiwa dayalisisi pamoja, jambo ambalo limetudhoofisha kifedha. Nimejitolea mwanangu aweze kufanyiwa pandikizi kwani ana familia changa,” alisema Bw Kimani.

Familia ilipata watu watano waliojitolea kuwa wafadhili wa figo, miongoni mwao akiwa kaka na mpwa wa Kiarie.

Kwa sasa wanahitaji Sh3.6 milioni ili kukamilisha oparesheni hiyo.

Wanaomba wasamaria wema na wahisani kujitolea kusaidia familia yake kupata pesa hizo.

Bw Stephen Kimani na Zacchaeus Kiarie. PICHA|MERCY KOSEKI
  • Tags

You can share this post!

Matimbo hatari ya Kimolwet yanameza watu hasa walevi

Aibu taulo za hedhi zilizotumika zikitapakaa mitaani Nairobi

T L