• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Mashirika, viongozi wa kidini wataka IEBC kuzingatia uadilifu uchaguzini

Mashirika, viongozi wa kidini wataka IEBC kuzingatia uadilifu uchaguzini

NA TITUS OMINDE

WANAHARAKATI wa kutetea haki za binadamu na viongozi wa kidini, wameionya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) dhidi ya kujihusisha na aina yoyote ya utovu wa nidhamu unaoweza kutatiza matokeo kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Wakiongozwa na mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Kibinadamu na Demokrasia (CHRD) Bw Kipkorir Ng’etich, viongozi hao walitoa changamoto kwa IEBC kuzingatia wajibu wake wa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Bw Ngetich anataka IEBC kukoma kujihusisha na siasa na kujitolea kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ambao utaepusha aina yoyote ya fujo zinazotokana na matokeo ya uchaguzi.

“IEBC lazima ikome kujihusisha na mambo ya kando pamoja na siasa ambazo zina uwezo wa kugeuza mwelekeo wao. Jukumu la IEBC ni kuhakikisha tuna uchaguzi huru na wa haki Agosti 9,” alisema Bw Ng’etich.

Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret, Ng’etich alijutia tukio la hivi majuzi ambapo raia wa Venezuela walikamatwa na vifaa vya uchaguzi.

Bw Ng’etich alisema wanaharakati wa haki za binadamu na viongozi wa kidini wanatatanishwa na madai yanayoibuka ya njama ya kuvuruga uchaguzi kufuatia kukamatwa kwa raia hao watatu wa Venezuela wakiwa na nyenzo za uchaguzi.

Kwa upande wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK), mwenyekiti wa baraza hilo katika North Rift Abubakar Bini alisema mvutano wa juzi kati ya IEBC na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuhusu kukamatwa kwa Wavenezuela hao watatu sio kiashirio kizuri kwa uchaguzi huru na haki.

Sheikh Bini alisema lazima IEBC izingatie uadilifu wa hali ya juu ili kuepusha mizozo baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

“IEBC daima imekuwa ikiwaambia Wakenya kwamba mikakati kabambe imewekwa ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki lakini kufuatia matukio ya hivi majuzi, tunaanza kutilia shaka ufaafu wa IEBC kuelekea uchaguzi huru na wa haki,” alisema Sheikh Bini.

Kwa upande wake, Askofu wa jimbo Katoliki la Eldoret Dominic Kimengich aliambia IEBC kujiepusha na tabia ambazo zinaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.

“Kama makasisi, tuna imani na IEBC kufanya uchaguzi wa kuaminika. Ushauri wangu kwa IEBC ni kwamba, ili Wakenya wote wawe na imani na shirika hilo, lazima IEBC ijiepushe na tabia ya kutiliwa shaka,” akasema Askofu Kimengich.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Umoja wa Pwani kusalia ndoto...

Sonko aacha Kalonzo mataani, ajiunga na Ruto

T L