• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Microsoft ADC yashirikiana na YALI kuwahami vijana na ujuzi

Microsoft ADC yashirikiana na YALI kuwahami vijana na ujuzi

NA LAWRENCE ONGARO

MASHIRIKA ya Microsoft Africa Development Centre (ADC) na Young African Leaders Initiative (YALI) yametia saini makubaliano ya ushirikiano wa kupokezana ujuzi wa masuala ya kidijitali na kiteknolojia.

YALI wana makao katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Washiriki chini ya mpango huo watapokea mafunzo kutoka kwa wataalam wa ADC.

Mkataba huo ulitiwa saini na mkurugenzi wa shirika la ADC ni Catherine Muraga na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) Prof Paul Wainaina.

Kulingana na mkataba huo, lengo kuu ni kwa wanafunzi kutoka nyanja zote kujiongezea maarifa ya maswala ya kidijitali, ubunifu wa kiakili, na pia jinsi ya kutumia vifaa vya kiteknolojia kwa kupewa mafunzo maalum.

Kulingana na mpangilio uliopo ni kwamba watakaopata fursa ya kupata maarifa zaidi kwenye mpango huo nao watasambaza maarifa hayo kwa vijana chipukizi.

Bi Muraga alitaja hatua hiyo kuwa ni ya kufana kwa sababu inalenga kubadilisha mtazamo wa vijana wengi barani Afrika.

“Ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu utaleta mabadiliko mengi hasa katika sekta ya teknolojia ambayo inakua kwa kasi. Tunafanya juhudi kuona ya kwamba yeyote anayetaka kupata maarifa anaondoka na ujuzi tele,” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema mafunzo hayo yakishika kasi yatakuwa na faida kwa watu wengi katika bara la Afrika na ulimwenguni kote ambapo pia uchumi utaimarika.

Kwa upande wake, Prof Wainaina alisema ushirikiano wa vijana kutoka bara la Afrika na shirika la ADC bila shaka utaleta mwanga zaidi kuhusu maswala ya kidijitali.

“Ni muhimu kupanga ushirikiano wa aina hiyo kila mara ili kuongezea vijana maarifa wanayohitaji katika ulimwengu wa sasa unaondeshwa zaidi kiteknolojia,” akasema Prof Wainaina.

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri ashtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh60 milioni

Maina Njenga ahojiwa na DCI, polisi watawanya wafuasi wake

T L