• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Miili iliyokuwa inatafutwa baada ya gari kusombwa na maji yapatikana

Miili iliyokuwa inatafutwa baada ya gari kusombwa na maji yapatikana

NA ALEX KALAMA

Miili miwili iliyokuwa ikitafutwa katika Mto Gwaseni huko Bamba eneo bunge la Ganze Jumatatu, Novemba 27, 2023 baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji, imepatikana leo Jumanne, na kufikisha jumla ya miili minne ambayo imeopolewa katika mto huo.

Akithibitisha taarifa hii, afisa wa majanga Kaunti ya Kilifi Japheth Chengo ameeleza kuwa, juhudi za idara ya majanga na kitengo cha moto zimefanikisha zoezi hilo, ambalo limechukua siku moja.

“Tumeweza kuipata ile miili miwili ya watu waliozama jana baada ya gari lao kusombwa walipojaribu kuvuka mto Gwaseni. Miili hiyo tumeweza kuipeleka katika chumba cha hifadhi ya wafu cha hospitali kuu ya Kilifi,” alisema Bw Chengo.

Aidha, Bw Chengo ameeleza kuwa mwili wa kijana aliyezama maji katika Mto Rare jioni ya Jumapili iliyopita, bado ungali unatafutwa, watu wanaoishi au kutumia barabara zilizoko karibu na mito wamehimizwa kuwa makini zaidi.

“Kwa sasa wapiga mbizi wetu pamoja wale wa majanga na wakishirikiana wadau wengine bado wamekita kambi katika Mto Rare wakiendelea kutafuta mwili wa kijana mmoja aliyesombwa na maji mnamo Jumapili.

“Pia nitoe tahadhari kwa wakazi wa Kilifi kwamba wawe waangalifu zaidi wanapotumia barabara zinazopita karibu na mito, ikiwezekana watafute sehemu zingine mbadala ili kujiepusha kupoteza maisha kwa sababu hivi sasa mito mingi imefurika,” alisema Bw Chengo.

Aidha, afisa huyo wa majanga amedokeza kuwa kufikia sasa Kaunti ya Kilifi imepoteza zaidi ya watu 13 kutokana na mvua ya El-Nino

  • Tags

You can share this post!

Homoni za kiume huwa chache kwa wanaume wasiolala vya...

Seremala kortini kwa dai la kuchafua mtoto, 12, na...

T L