• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
MKU yakariri kujitolea kuendelea kushiriki makongamano ya uimarishaji wa elimu

MKU yakariri kujitolea kuendelea kushiriki makongamano ya uimarishaji wa elimu

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kiliandaa kongamano lililoleta pamoja washiriki kutoka kwa vyuo vya mataifa saba.

Jumla ya wageni wapatao 1,000 walikongamana katika ukumbi wa MKU mjini Thika kuanzia Mei 22 hadi Mei 26, 2023.

Naibu Chansela wa MKU Prof Deograttius Jaganyi alisema kongamano la kwanza la Access Summer School lilifanyika mara ya kwanza nchini Ghana na la pili likaandaliwa Benin.

Vyuo sita vya bara Afrika vilikuwa ni MKU ya Kenya na vingine kutoka Benin, Ghana, Nigeria, Rwanda, na Tunisia. Cha saba kilikuwa Chuo Kikuu cha Leipzig kutoka Ujerumani.

Makongamano ya Summer School hujikita katika kuimarisha majadiliano, kuangazia mtaala wa masomo, na kujadili ushirikiano baina ya serikali mbalimbali na taasisi za elimu.

Mgeni wa heshima katika hafla hiyo Prof Dickson Andala ambaye amebobea katika masuala ya utafiti, alisema wanafunzi wanaotafuta ajira baada ya kuhitimu wanastahili kuwa na ujuzi wa hali ya juu.

Alitoa changamoto kwa wanafunzi waimarishe ubunifu wao ili waweze kupata ajira au kubuni nafasi za kazi.

“Tunaelewa dunia ya sasa ni ya kidijitali na kwa hivyo ni vyema kuangazia mawazo yetu katika mwelekeo huo,” alisema Prof Andala.

Msomi huyo aliwahimiza wanafunzi kutafuta nafasi za kujiendeleza kwa masomo ya juu kama uzamili na uzamifu, ili kuwawezesha kupata ajira katika soko la ajira lenye ushindani mkali.

Aliongeza kwamba kuna haja kubwa ya wanafunzi Waafrika kupata nafasi za kujiendeleza zaidi kielimu.

Aidha, Prof Andala alipongeza MKU kwa kuyapa maswala ya utafiti kipaumbele. Naibu Chansela Prof Jaganyi yuko katika mstari wa mbele kuwafadhili wanafunzi na fedha za kufanya utafiti. Prof Andala alirai MKU kuendelea kuwainua wanafunzi wengi.

MKU imepongezwa kwa kushirikiana na chuo kimoja cha nchini Ujerumani na kuwatuma wauguzi kadha kwenda kusomea elimu ya maswala ya afya ambapo watapata ajira katika nchi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Rais Biden aanguka baada ya kuongoza hafla ya kufuzu kwa...

AK yaitisha mkutano na makocha wakune vichwa jinsi ya...

T L