• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Mlima Kenya walia kupanda kwa gharama ya maisha licha ya kuwa ngome ya Kenya Kwanza

Mlima Kenya walia kupanda kwa gharama ya maisha licha ya kuwa ngome ya Kenya Kwanza

Na WAANDISHI WETU

KUPANDA kwa gharama ya maisha na pia bei ya mafuta kumewagawanya viongozi na wakazi wa Mlima Kenya ambao sasa wametishia kuondoa uungwaji mkono kwa utawala wa Kenya Kwanza.

Wakazi wa Mlima Kenya waliipigia kura Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua kwenye uchaguzi mkuu uliopita na eneo hilo linafahamika kama ngome ya kisiasa ya viongozi hao wawili.

Hata hivyo, kupanda kwa bei ya mafuta kumechemsha eneo hilo japo viongozi waliochaguliwa wanahofia kujitokeza hadharani wasionekana wanapinga serikali.

Kwa upande mwingine, wakazi na viongozi wa miungano ya kibiashara na wahudumu wa bodaboda nao wanalalamikia kuwa mambo yamewaendea segemnege huku wakitaka serikali irejeshe ruzuku ili kushushwa bei ya mafuta.

“Hii serikali haiwajali raia tena. Rais William Ruto anastahili kurejesha ruzuku jinsi alivyofanya mtangulizi wake Rais Uhuru Kenyatta ili kushusha bei ya mafuta. Iwapo bei ya mafuta itakuwa chini, pia bei ya bidhaa za kimsingi pia zitapungua,” akasema Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili tawi la Laikipia Robert Miano.

Mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda Laikipia Silas Kimathi naye alisema kuwa sekta ya uchukuzi imeathirika vibaya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

“Nawajua wahudumu wa bodaboda ambao wameacha kazi zao na sasa wanafanya vibarua kwenye maeneo ujenzi unaendelea. Wamefanya hivyo kwa sababu hawawezi kumudu gharama ya kununua mafuta,” akasema Bw Kimathi huku akikashifu serikali kwa masaibu hayo.

Baadhi ya wabunge wa UDA ambao walizungumza na Taifa Leo waliomba majina yao yabanwe ila wakakiri kuwa Kenya Kwanza huenda ikapoteza uungwaji mkono mlimani kwa sababu wakazi wanaumia mno kiuchumi.

“Hali si nzuri kabisa kwa sababu watu ambao walituchagua wanaumia. Sitaki ninukuliwe ila huu ndio ukweli wa mambo. Lazima kitu kifanyike kuokoa hali,” akasema Mbunge mmoja wa UDA ambaye aliomba jina lake libanwe.

Diwani wa wadi ya Segera Kaunti ya Laikipia Salim Edung naye alitetea utawala wa sasa akisema unahitaji upewe muda zaidi ili kuhakikisha kuwa uchumi utakuja kuwa dhabiti.

Katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, wakazi walikashifu vikali Kenya Kwanza kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta. Mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda Evans Kinoti hata alitishia kuwaongoza wenzake kuandaa maandamano ya kushinikiza serikali ipunguze bei hiyo.

“Tulimchagua Rais William Ruto kwa sababu alituahidi kuwa anaelewa shida za wananchi ila kwa sasa mambo ni kinyume,” akasema Bw Kinoti.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Multimedia Profesa Gitille Naituli alimtaka Rais Ruto aaondoe ushuru kwenye mafuta ila ashushe chini ugumu wa maisha unaoshuhudiwa kwa sasa.

Mhudumu wa bodaboda Steven Kimani ambaye anaishi mjini Murang’a naye alisema kuwa amewakosa wateja baada ya wao kusaka njia nyingine za kusafiri. Hii ni baada ya kuongeza nauli wanayotoza kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Askofu wa Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria naye amesema kuwa bei ya juu ya mafuta itaongeza kiwango cha umaskini nchini.

Ripoti ya JAMES MURIMI, GITONGA MARETE, MWANGI NDIRANGU, ALEX NJERU na MARTIN MWAURA

  • Tags

You can share this post!

Waititu, mkewe Susan wana kesi ya kujibu katika kashfa ya...

Polisi wasaka mwanamke mshukiwa wa mauaji aliyenaswa...

T L