• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:34 PM
Mmoja auawa kwenye mzozo kuhusu vijana wawili

Mmoja auawa kwenye mzozo kuhusu vijana wawili

Na GEORGE MUNENE

Mtu mmoja ameuawa  kwa risasi huku taharuki ikizidi kutanda mjini Kianjokoma, Kaunti ya Embu kufuatia mauaji ya vijana wawili.

Wakati huo huo, Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusu vifo vya kaka hao wawili waliopatikana wakiwa wamefariki baada ya kukamatwa na polisi wakati wa saa za kafyu.

Mamia ya wakazi wa Kianjokoma walianza kutoroka eneo hilo baada ya serikali kuwatuma maafisa zaidi kutoka kaunti jirani za Makueni na Machakos ili kurejesha utulivu.

Maafisa wa polisi waliojihami vikali walifika mjini humo asubuhi na kuanza kupiga doria mitaani hali iliyowafanya wakazi kutoroka kwa hofu.

Taifa Leo ilibaini kuwa majengo mengi ya kibiashara yamefungwa na wamiliki wake kutorokea kusikojulikana wakihofia kukamatwa.

IPOA iliahidi kufanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini ni nini hasa kilichotendeka. Baada ya kukamilisha uchunguzi, IPOA itatoa mapendekezo ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa kwa wahusika ikiwa itabainika kwamba maafisa wa polisi walichangia kwa njia ya uhalifu.

Kupitia taarifa, mwenyekiti wa IPOA, Anne Makori, aliwahakikishia jamaa na familia za wahasiriwa kuhusu uchunguzi wa haki na usioegemea upande wowote.

Kulingana na familia hiyo, Benson Njiru 22 na Emmanuel Mutura 19, ambao walikuwa wanafunzi wa chuo walikamatwa na polisi Jumapili usiku, umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwa madai ya kukiuka kafyu.

Miili yao ilipatikana baadaye MochariWazazi wao, John Ndwiga na Catherine Wawira walisema walishtuka walipofahamishwa kuhusu vifo vya watoto wao huku wakililia haki.

Walidai kuwa watoto wao waliuawa na polisi na miili yao ikapelekwa mochari kisiri bila kuwafahamisha ili kuficha ushahidi.

Vijana hao walipotoweka, jamaa zao walianzisha msako mkali bila mafanikio kabla ya kuandikisha ripoti katika Kituo cha Polisi cha Manyatta ambapo maafisa walionekana kusitasita kuwasaidia.

” Tulipowasili katika kituo hicho, maafisa walituzungusha bila kutueleza ni wapi walipo watoto wetu. Hatuna furaha hata kidogo,” alisema Bw Ndwiga.

You can share this post!

Ni kisasi, vita vya ubabe kati ya Faith na Hassan fainali...

Uhuru ajaza nafasi nne za makamishna wa IEBC