• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
Mombasa Cement na NMG zashirikiana kuinua elimu Kilifi kupitia mradi wa NiE

Mombasa Cement na NMG zashirikiana kuinua elimu Kilifi kupitia mradi wa NiE

Na WACHIRA MWANGI

SHULE kadhaa katika Kaunti ya Kilifi zimepongeza ushirikiano kati ya Shirika la Habari la Nation (NMG) na Kampuni ya kutengeneza saruji ya Mombasa Cement, kupitia Mpango wa Matumizi ya Magazeti Kufundishia (NIE).

Kulingana na walimu, wazazi na wanafunzi. mpango huo umechangia kuimarika kwa matokeo yao kwenye mitihani ya kitaifa.Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mtondia, Wilson Omwansu asema kupitia magazeti ya ‘Daily Nation’ na “Taifa Leo” yanayowasilishwa shuleni humo kila wiki, wanafunzi wamependa kusoma na kuimarisha umilisi wao wa lugha za Kiingereza na Kiswahili.

“Magazeti haya yametusaidia kuimarisha utamaduni wa kusoma miongoni mwa wanafunzi wetu. Wamepata hamu ya kusoma zaidi kwa usaidizi wa picha na michoro. Walimu pia wameimarisha uelewa wao wa matukio ya kila siku ambao wanaupitisha kwa wanafunzi.

“Jarida la ‘Junior Spot’ katika gazeti la ‘Daily Nation’ na mitihani ya majaribio yanayochapishwa katika ‘Taifa Leo’ pia yamesaidia shule yetu kuimarika katika alama ya wastani kwenye mitihani ya kitaifa,” Bw Omwansu akasema huku akihimiza kuwa mpango huo uendelee.

Mpango wa NIE ulianzishwa chini ya mwavuli wa mradi wa “Young Reader Development” unaohusu matumizi ya magazeti kama vyombo vya kufundishia katika kiwango cha shule za msingi na upili.

Mpango huo unaotekelezwa na kampuni ya NMG pia unalenga kuimarisha uhamasisho kuhusu uraia mwema miongoni mwa watoto kupitia usomaji magazeti.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Mtondia, Bi Fundi Mwalukumbi alisema shule yake ina wanafunzi wengi na akahimiza kuwa iwe ikitengewa idadi kubwa ya magazeti mpango wa NIE utakaporejelewa.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Bofa, Bw Zepplin Mwanyae alisema wamefaidi pakubwa kutokana na uwasilishaji wa magazeti katika shule hiyo.

“Shule yetu imeongeza alama zaidi alama zake za wastani katika mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) kutokana na mitihani ya majaribio ambayo imekuwa ikichapishwa katika gazeti la ‘Taifa Leo’. Tunahimiza kuwa mpango huu muhimu uendelezwe kwa manufaa ya watoto wetu na jamii kwa ujumla,” Bw Mwanyae akasema.

Mhariri Mkuu wa “Taifa Leo”, Bw Peter Ngare alisema azma kuu ya mradi wa NIE ni kuchochea desturi ya usomaji miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na upili kote nchini, pamoja na kusaidia kuwaandaa kwa ajili ya kupita mitihani.

‘Usomaji huchangia sana katika ustawi wa jamii yoyote ile, ndiposa kama NMG tuna mchango wa kuhimiza watoto wetu kupenda kusoma na kuendelea hata baada ya kumaliza shule,’ akasema Bw Ngare.

Alisema NMG itaendelea kuwekeza katika mradi huo kama sehemu ya mchango wake kwa jamii.Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo na Uhusiano Mwema wa NMG, Bw Clifford Machoka naye alieleza kuridhishwa na ushirikiano ambao umekuwepo kati ya NMG na Mombasa Cement, ambao umesaidia katika kuhakikisha magazeti yanafikia shule nyingi eneo la Pwani.

‘Mombasa Cement imetambulika kote Pwani kwa kusaidia katika kuinua jamii kupitia miradi kama vile maji, chakula, ujenzi wa shule na mazingira. Tangu tuanze kushirikiana nao tumefanikiwa kufikia shule nyingi kwa magazeti, na matokeo yake yamejidhidhirisha kwa kuimarisha ubora wa masomo katika shule zinazofadhiliwa,’ akaeleza Bw Machoka.

Afisa wa Mauzo anayehusika na mradi wa ‘Taifa Leo’, Bw Nuhu Bakari alisema kuwa kupitia mpango huo, wameweza kukuza talanta, kuwapa wanafunzi motisha ya kudurusu, kuimarisha uwezo wao wa kuandika kupitia mashindano ya uandishi wa insha kwa zaidi ya miaka mitano.

“Kando na nyanja ya elimu, mpango wa NIE pia unaimarisha uwezo wa watoto kuandika, kusoma na kutumia lugha za Kiswahili na Kiingereza.Tunahudumia kaunti zote 47 kupitia magazeti ya ‘Taifa Leo’ na mpango wetu wa kuimarisha uwezo wa wanafunzi kusoma kwa sauti na hadharani,’ akaongeza Bw Bakari.

You can share this post!

Serikali yazima Mt Kenya TV kwa kupotosha watoto

WANDERI KAMAU: Raila ni mdau wa kipekee katika historia ya...