• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Mpesa ya mwanaharakati wa ushoga Chiloba ilitumika kulipia jeneza na teksi, korti yaambiwa

Mpesa ya mwanaharakati wa ushoga Chiloba ilitumika kulipia jeneza na teksi, korti yaambiwa

NA TITUS OMINDE

SHUGHULI zote za kifedha zinazohusishwa na mauaji ya mwanaharakati wa masuala ya ushoga (LGBTQ), Edwin Kiptoo almaarufu Chiloba, zililitekelezwa kupitia M-pesa kwa kutumia simu ya marehemu.

Shahidi kwenye kesi hiyo ambaye alimuuzia mshukiwa mkuu Jackton Odhiambo sanduku la bati, alieleza mahakama ya Eldoret kuwa alilipwa kupitia M-pesa ya simu ya marehemu.

Sanduku hilo lilitumika kusafirisha mwili wa Chiloba kabla ya kutupwa viungani mwa mji wa Eldoret kati ya Desemba 2022 na Januari 2023.

Bw Obadiah Ochieng alimweleza Jaji Reuben Nyakundi, kuwa mshtakiwa ambaye alikuwa anamfahamu, alimtembelea kazini kutafuta sanduku la bati.

Alimuonyesha Odhiambo bidhaa zake zikiwa ni aina mbalimbali za masanduku maridadi, ambapo alisisitiza kuwa alitaka sanduku kubwa la bati.

Kwa kuwa Bw Ochieng hakuwa na sanduku la bati alilohitaji mteja wake, alimpeleka kwenye karakana iliyo karibu ambayo ilisambaza baadhi ya bidhaa zake.

Alipofika kwenye karakana hiyo, mshtakiwa alivutiwa na mojawapo wa masanduku makubwa ya bati kwenye rafu.

‚ÄúSanduku hilo lilipakwa rangi ya kijani kibichi. Mimi ndiye niliyelitengeneza na nilimuuzia kwa sh 7,500,” Bw Ochieng’ alisimulia mahakamani.

Alimsaidia kulipakia kwenye gari alilokuwa akiendesha.

Dereva wa teksi ambaye alitoa gari lililotumiwa kubeba mwili wa Chiloba, aliambia mahakama kwamba, yeye pia alilipwa kupitia M-Pesa baada ya kutoa gari lake kwa Bw Odhiambo ambaye alijiendesha mwenyewe.

Mashahidi wote wawili waliotoa ushahidi mbele Jaji Nyakundi, walisimulia jinsi mshtakiwa almaarufu Lizer alivyowalipa kwa huduma zao kupitia M- pesa.

Bw Francis Were, ambaye ni dereva wa teksi, alisema kwamba alikodisha gari la Toyota fielder KCL 229L kwa Bw Odhiambo ambaye alikuwa radfiki yake tangu utotoni.

Bw Were aliambia mahakama kuwa Bw Odhiambo, mtoto wa kasisi moja mjini Eldoret, aliomba kukodisha gari lake Januari 3 mwaka huu, alimweleza kuwa ana shughuli ya kuhudhuria kanisani.

Baadaye Bw Were alikamatwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya mwanaharakati huyo.

Bw Odhiambo ameshtakiwa kwa kumuua Bw Chiloba kati ya Desemba 31, 2022 na Januari 3, 2023 katika Noble Breeze Apartment mtaani Chebisaas kaunti ndogo ya Moiben.

Mwili wa Chiloba ulipatikana umeingizwa kwenye sanduku la bati kando ya barabara ya Kipkenyo-Kaptinga kata ya Mukombet viungani mwa mji wa Eldoret mnamo Januari 4, 2023.

Tukio hilo lilivuta hisia za kimataifa, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, akiitaka serikali ya Kenya kuharakisha uchunguzi na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.

Kesi hiyo itaendelea kusikizwa Jumatano, Novemba 22.

  • Tags

You can share this post!

Afisa wa polisi aelekeza mtutu wa bunduki mdomoni na...

Kocha Firat asema Harambee Stars imeiva sasa huku Omala...

T L