• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Mpishi mwenye ulemavu wa macho atupwa jela miaka 30 kwa kumnajisi mtoto

Mpishi mwenye ulemavu wa macho atupwa jela miaka 30 kwa kumnajisi mtoto

NA TITUS OMINDE

MPISHI mmoja wa shule ya msingi ya kibinafsi mwenye ulemavu wa macho, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri kosa la kumnajisi mwanafunzi wa shule ya chekechea mwenye umri wa miaka mitano.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 20 alishangaza mahakama ya Eldoret mnamo Jumatano alikiri kwamba harakati zake za uovu alifanyia katika darasa la shule ambapo mshtakiwa amekuwa akifanya kazi ya upishi pamoja na mamake mwathiriwa.

Mshtakiwa alidai kuwa tayari alikuwa ameshamvua mtoto huyo suruali ndipo mama yake “alinikuta eneo la tukio ila sikuwa nimemnajisi”.

Alishikilia kuwa hakuwa amefanya kitendo chenyewe wakati mama wa mtoto huyo alifika eneo la tukio.

Karatasi ya mashtaka ilisema kuwa mshtakiwa alimnajisi mtoto huyo ndani ya darasa katika shule ya kibinafsi katika kaunti ndogo ya Moiben mnamo Agosti 29, 2023.

Vile vile alikabiliwa na shtaka mbadala la kufanya kitendo kichafu na mtoto kinyume na sheria ya Makosa ya Mapenzi ya mwaka 2006.

Taarifa ya mtoto huyo mahakamani ilithibitisha kwamba alinajisiwa na mshtakiwa ambaye alikuwa anamfahamu.

“Aliniita darasani na kunivua soksi kabla ya kuniweka kwenye meza ya mwalimu baada ya kufungua zipu ya suruali yake na kunifanyia tabia mbaya,” ilisema taarifa ya mtoto huyo mahakamani.

Yamkini mshtakiwa alikiri mashtaka walakini alidai kuwa ingawa alimvua chupi mtoto huyo, hakumnajisi.

“Nilikuwa nimemvua chupi na mama yake alipoingia akipiga kelele nilitoka darasani mbio kwa sababu mzazi huyo alikataa kunisikiliza ili tuzungumzie suala hilo na kulitatua papo hapo,” mshtakiwa aliiambia mahakama akijitetea.

Mshtakiwa alikamatwa baadaye na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Ainabtich.

Alikamatwa siku iliyofuata katika eneo la Mti Moja mjini Eldoret alikokuwa amekimbilia baada ya kisa hicho kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Ainaptich.

Ripoti ya uchunguzi wa kimatibabu kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) ilionyesha kuwa mtoto huyo alinajisiwa.

Alipokuwa akitoa uamuzi wake, Hakimu Mwandamizi wa Eldoret Caroline Wattimah alibainisha kuwa hata kama mshtakiwa alidai kwamba hakuwa amemnajisi mtoto huyo mamake alipoingia, hatua yake ya kumvua nguo ilikuwa dhihirisho la wazi kwamba alikuwa na nia mbaya.

“Kitendo chako na maelezo yako mwenyewe yamethibitisha kuwa wewe si mtu mzuri na zaidi, kwa mtoto mdogo aliyekujua. Mahakama hii inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela,” akaamuru hakimu.

Mshtakiwa ana siku 14 za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Tanzania yakana madai ya ulanguzi wa wanyamapori kutoka...

Mchungaji mifugo akiri kumchafua ng’ombe kukata kiu ya...

T L