NA MERCY KOSKEI
POLISI katika Kaunti ya Nakuru wanamzuilia mshukiwa wa mauaji ya kutisha ya msichana mwenye umri wa miaka 12 ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa kwenye kichaka.
Jasmine Njoki, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Roots Academy, anadaiwa kuvamiwa na wahuni waliomnajisi kabla ya kumuua alipokuwa akielekea nyumbani mwendo wa saa kumi na moja.
Mwili wake ulipatikana kichakani, karibu mita mia 800 kutoka nyumbani kwao.
Kulingana na Mkuu wa Upelelezi Kitengo cha Jinai Kaunti Ndogo ya Gilgil, Bw David Ochieng, mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 21 alikamatwa wiki iliyopita na majasusi na kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, alipofikishwa kortini Naivasha, wapelelezi waliomba siku kumi zaidi ili kukamilisha uchunguzi.
“Mshukiwa alifikishwa mahakamani. Kwa sasa yuko chini ya ulinzi akitusaidia na uchunguzi zaidi. Tunasaka washukiwa wengine kuhusiana na mauaji hayo,” afisa huyo alisema.
Jasmine alizikwa mnamo Jumatano, Septemba 28, 2023 katika hafla iliyoleta pamoja familia, marafiki na jamii katika kijiji cha Kasambara, huku wito wa haki ukiwa ajenda kuu.
Mamake Jasmine, Bi Trizah Wangari ambaye alizungumzia waombolezaji akionekana kusawijika na kifo cha msichana Jasmine, alimtaja bintiye ambaye ni mzaliwa wa kwanza kama rafiki wa karibu akisikitika maisha ya mwanawe kukatizwa mapema.
Alisema kuwa kwa kipindi kifupi walichojaaliwa kukaa na Jasmine, alikuwa msichana mtiifu na mwenye heshima.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa zawadi hiyo japo kwa muda mfupi. Nilijaribu kila niwezalo kuwa mama bora kwako na kutekeleza jukumu langu vizuri katika kukuongoza na kukulinda. Nina huzuni kukupa buriani,” aliomboleza.
Babake Jasmine, Francis Wambugu alisema kuwa “Ni vigumu kuamini kwamba umetuacha, kifo chako kimeleta huzuni kubwa kwa sababu tumepoteza msichana mahiri na binti ambaye alitupenda siku zote.”
Viongozi wa kisiasa na kidini waliohudhuria mazishi hayo, walilaani vikali mauaji ya msichana huyo na kutaka polisi kuhakikisha haki inatendeka.
Gavana wa Nakuru, Bi Susan Kihika alisema kuwa inasikitisha kuwa ni mshukiwa mmoja tu ametiwa mbaroni huku akiwataka wachunguzi kumhoji mshukiwa kwa kina ili kufichua wahalifu wengine.
Mbunge wa Gilgil, Bi Martha Wangari alisema kuwa kituo cha polisi kitajengwa katika eneo hilo ili kuhakikisha maafisa wanapiga doria kila siku.