NA COLLINS OMULO
WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu amesema familia za wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Sacred Heart Mukumu walioaga dunia baada ya kula chakula kibovu na kunywa maji machafu zitapokea fidia ya Sh400,000 kwa kila mwanafunzi aliyeangamia.
Bw Machogu ambaye anahojiwa na Seneti amesema mpango huo utafanikishwa na bima ya afya ya EduAfya.
Vile vile amesema kwamba wizara iligharimia matibabu ya wanafunzi 109 waliolazwa baada ya kula chakula kibovu.
Akielezea kuhusu idadi ya wanafunzi waliorejea shuleni hadi kufikia sasa, waziri amesema wanafunzi 1,962 wamerejea shuleni, 44 bado hawajaripoti shuleni na 56 wametuma maombi waruhusiwe kuenda kusomea katika shule nyingine.
“Kufikia sasa hatuna ripoti zozote za kutuwezesha kumtuhumu yeyote kwa kutelekeza majukumu yake. Hali ilivyo sasa ni vigumu kumpeleka yeyote kortini kushtakiwa,” amesema waziri Machogu.
Mnamo Jumamosi iliyopita waziri Machogu alizindua rasmi kituo kilichojengwa kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kuchota na kunywa maji safi.
Mpishi mmoja akihojiwa na wanahabari wa Taifa Leo waliozuru shule hiyo alidai walikuwa wakiletewa nyama iliyoharibika na kulazimishwa kuipika.
Wanafunzi wanne walipoteza maisha. Vile vile mwalimu mmoja aliangamia baada ya viungo vyake muhimu kukataa kufanya kazi.