• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 12:33 PM
Muturi ajipata solemba mwaka mmoja baada ya kusaidia Kenya Kwanza kuingia mamlakani

Muturi ajipata solemba mwaka mmoja baada ya kusaidia Kenya Kwanza kuingia mamlakani

NA MOSES NYAMORI

MSWADA mpya wa kufanyia marekebisho Sheria kuhusu Usimamizi wa Serikali ya Kitaifa 2023 uliowasilishwa katika Bunge la Kitaifa kwa mara nyingine umeibua mvutano unaotokota katika Idara ya Sheria Nchini.

Taifa Leo imebaini kuhusu juhudi za kumpunguzia mamlaka Mwanasheria Mkuu Justin Muturi huku ripoti zikiashiria kwamba baadhi ya miswada ya serikali haipitishwi kwake.

Pendekezo la kuondoa wajibu wake kama msimamizi wa mhuri wa umma limejumuishwa katika Mswada mpya ambao duru zinasema, uliandaliwa pasipo mchango wake kama mshauri mkuu wa serikali kuhusu sheria.

Mswada huo uliowasilishwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, unadhamiriwa kuhamisha mamlaka kwa Mkuu wa Huduma ya Umma, wadhifa unaoshikiliwa kwa sasa na Felix Koskei.

“Mkuu wa Watumishi wa Umma atakuwa – mkuu wa wafanyakazi kwa Rais, msimamizi wa Afisi ya Rais, msimamizi wa Mhuri wa Umma na vifaa vinginevyo vya Serikali ambavyo havisimamiwi na mtu yeyote,” unapendekeza Mswada.

Bw Muturi vilevile yupo kwenye mvutano mwingine wa mamlaka na Wakili wa Serikali Shadrack Mose na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC).

Imeibuka kuwa Bw Mose anapimana nguvu na Bw Muturi katika Idara ya Sheria kwa kuripoti moja kwa moja kwa Rais William Ruto.

Kwa kawaida, Mwanasheria Mkuu ndiye husimamia na kusambaza majukumu kwa Wakili wa Serikali lakini imeibuka kuwa wawili hao sasa wanashindana kujibu moja kwa moja kwa Rais.

Bw Muturi hakujibu maswali yetu kuhusu ripoti zinazosema alitengwa wakati wa kunakili Mswada wa Kufanyia Marekebisho Sheria kuhusu Usimamizi wa Serikali Kuu 2023.

Hata hivyo, hapo awali amekanusha kuwapo mvutano wowote wa mamlaka kati yake na Bw Mose.

Wakati huo vilevile, wabunge wamevutwa kwenye makabiliano makali kati ya Bw Muturi na PSC kuhusu ajira na kupandishwa mamlaka kwa mawakili wakuu.

PSC imewaagiza wabunge kutupilia mbali pendekezo la kufanyia marekebisho Sheria kuhusu Afisi ya Mwanasheria Mkuu, 2012 inayolenga kupatia afisi hiyo mamlaka ya kuteua Naibu Wakili wa Serikali na Wakili wa Serikali.

  • Tags

You can share this post!

Mume anaishi mjini na miye huku mashambani, nahofia...

‘Wagathanwa’ aendelea kushambulia wakazi licha ya...

T L