SHANGAZI;
Mpenzi wangu ni mwalimu na anaishi mbali. Nimeshangaa sana kupata ujumbe kutoka kwake akisema kuwa ana mimba. Hatujaonana kwa mwaka mzima na ninaamini mimba hiyo si yangu. Naomba ushauri wako.
Iwapo kweli hamjaonana kwa mwaka mzima, mimba hiyo ni ya mwanamume mwingine. Hiyo ni changamoto kubwa kwa wapenzi wanaokaa muda mrefu bila kuonana. Jaribu kuzingatia jambo hili katika uamuzi ambao utachukua kuhusu uhusiano wenu.
Nina miaka 46. Kuna mwanamume anayeniambia ananipenda. Ana umri wa miaka 32. Ameteka hisia zangu pia lakini naona aibu kwa sababu ya umri wake. Ameniambia hiyo kwake si shida. Waonaje?
Watu wakipendana umri haufai kuwa kikwazo. Huyo ni mtu mzima na ameungama kuwa anakupenda licha ya umri wako. Kama wewe pia unampenda na unaamini anatosha kuwa mume wako, ondoa wasiwasi.
Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa. Nampenda sana mpenzi wangu na ninaamini yeye pia ananipenda. Lakini nahisi kuwa haniamini na hali hiyo inanisumbua moyoni. Naomba ushauri wako.
Sijui ni dalili gani ambazo umeona kwa mwenzako za kuonyesha kuwa hakuamini. Kama hajalalamika kuhusu uaminifu wako kwake, labda unamshuku bure tu. Ili kuondoa hofu, unaweza kumwelezea unavyohisi.
Mwanamume mpenzi wangu aliachishwa kazi mwaka uliopita. Nilijitolea kumsaidia nikidhani atatafuta kazi nyingi lakini sioni juhudi zozote. Naomba ushauri wako.
Mwanamume ndiye aliye na jukumu la kumtunza mwanamke, awe ni mpenzi ama mke wake. Utaamua iwapo uko tayari kuendelea kubeba mzigo huo sasa na baadaye kama atakuwa mume wako.