• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Mzee arushwa jela kwa ulaghai wa shamba

Mzee arushwa jela kwa ulaghai wa shamba

Na RICHARD MUNGUTI

MZEE wa miaka 60 atakula maharagwe kwa miaka mitatu gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ulaghai wa shamba mjini Nanyuki, Laikipia miaka minne iliyopita.

Gabriel Njoroge Mbuthia alifungwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi.

Bw Ochoi aliyempata na hatia Mbuthia ya kughushi cheti cha umiliki wa shamba la John Edward Njeru Thindayo, alisema ulaghai wa mashamba ulitibua uhasama mkali baina ya wahasiriwa na mlaghai.

Mbuthia alipatikana na hatia ya kumpora Thindayo shamba lenye ukubwa wa ektari 0.0394 mnamo  Julai 21, 2009 akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini.

Hakimu alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na James Gachoka, ulithibitisha kwamba Mbuthia alighushi cheti cha umiliki wa shamba hilo la Thindayo akiwa na nia ya kumpokonya.

Mbuthia alikamatwa katika afisi za Kaunti ya Nairobi alipodai cheti hicho cha shamba hilo kilikuwa chake.

Mbuthia alisisitiza cheti hicho kilikuwa halisi na kwamba kilitayarishwa na kutiwa sahihi na Afisa wa Usajili wa Mashamba eneo la Nanyuki kabla ya kukabidhiwa.

Baada ya kupatikana na hatia mshtakiwa aliomba msamaha akisema “umri wangu ni mkubwa na nitatesekea jela sana.”

Mshtakiwa aliomba akabidhiwe kifungo cha nje lakini hakimu akamweleza makosa aliyofanya ya kumpokonya mtu shamba ni mabaya na yanastahili adhabu ya kifungo kikavu gerezani bila faini.

“Nimetilia maanani ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka na nimekupata na hatia ya kughushi cheti cha umiliki wa shamba la mtu mwingine,” Bw Ochoi alisema akipitisha hukumu.

Bw Ochoi alisema suala la mashamba huzua uhasama mkali na hata wakati mwingine makabiliano na mauaji hutendeka mmoja akitetea shamba lake.

Hakimu alisema mahakama hazitasita kuwachukulia hatua kali walaghai wa mashamba.

Mshtakiwa alipewa siku 14 kukata rufaa ikiwa hakuridhika na uamuzi huo wa kufungwa miaka mitatu.

Mshtakiwa aliinamisha kichwa aliposikia hukumu ikitangazwa na hatimaye akaziba uso na viganja vya mkono.

  • Tags

You can share this post!

Ntalami aomboleza kifo cha mbwa wake

Maporomoko yaua wanaume wawili wakilala pangoni Mama Ngina

T L