NA VITALIS KIMUTAI
NAIBU Gavana wa Kericho, Bw Fred Kirui, amempa masharti mapya bosi wake Gavana Eric Mutai, ambayo anasisitiza lazima yatimizwe ili afanye naye kazi bila uhasama wowote.
Hii ni licha ya wawili hao kupatanishwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua hivi majuzi.
Bw Mutai anataka maafisa sita wa kaunti waliohusishwa na ubadhirifu wa Sh14.5 milioni za mchango ulioongozwa na Bw Gachagua miezi miwili iliyopita, wajiuzulu kutoka nyadhifa zao.
Pesa hizo zilikuwa zikichagiwa familia za watu 77 walioangamia kwenye ajali mbaya ya barabarani kule Londiani.
Ni wiki mbili zilizopita ambapo Bw Gachagua aliwakashifu wanasiasa hao wawili kwa uhasama baina yao, akisema unaathiri utekelezaji wa huduma kwa wananchi.
Mnamo Septemba 11, gavana na naibu wake walitangaza kuwa wamezika tofauti zao kisiasa na wapo tayari kufanya kazi pamoja.
Hii ni baada ya Bw Gachagua kuwatishia na kuwapatanisha mnamo Septemba 8, 2023.
Bw Gachagua aliwaambia wawili hao kuwa wasiporidhiana basi huenda wakaondolewa kwenye nyadhifa zao.
Hata hivyo, Bw Kirui sasa amesema kuwa lazima apate mgao wake ndani ya serikali jinsi alivyoahidiwa alipokubali kumwachia Bw Mutai tikiti ya kuwania ugavana wakati wa mchujo wa UDA kuelekea uchaguzi mkuu mwaka jana.
“Tulikuwa na mkataba ambao tulitia saini na Gavana nilipokubali kumwachia kiti kuelekea mchujo wa UDA,” akasema Mhandisi Kirui.
Alifichua kuwa iwapo matakwa yake hayataridhiwa basi yupo tayari kurejea kwa wananchi na kutatiza uongozi wa bosi wake.
“Mkataba wetu lazima uheshimiwe na utekelezwe ili mambo yawe sawa. Kwa sasa nashauriana na wazee na viongozi wa kidini kuhusu suala hili. Tuliporidhiana hivi majuzi, haikumaanisha kuwa nimeacha kile napigania na kushinikiza,” akaongeza.
“Mimi sivumilii ufisadi na sitafanya kazi na watu ambao ni mafisadi. Nataka kuhakikisha kuwa pesa ya mlipaushuru imetumika,” akasema.
Kiongozi wa Wengi kwenye Seneti Aaron Cheruyot ameingilia suala hilo, akisema inakuwa vigumu kupatanisha Gavana na Naibu wake.
Bw Cheruiyot amesema hali hiyo inasawiri kaunti hiyo vibaya na inaathiri utendakazi kwa raia.
“Kuwapatanisha imekuwa vigumu japo hatujakata tamaa. Tutajaribu mara ya mwisho kisha ikishindikana tutawaacha hivyo,” akasema.
Uhasama kati ya wawili hao ni bayana umechochewa na Gavana Mutai kukataa kutekeleza makubaliano kuwa wangegawa serikali, asilimia 60 za nyadhifa zikiendea Gavana na asilimia 40 kwa Bw Kirui.
Bw Cheruiyot na Kasisi Joyce Tonui wa Kanisa la Gospel ndio waliongoza mchakato wa juhudi za mwanzo kupatanisha wawili hao mwaka jana, 2022.
“Nimemtengea Naibu wangu nyadhifa kadhaa ikiwemo kuwa kiongozi wa wizara mbalimbali, shughuli za serikali na mwenyekiti wa kamati za baraza la mawaziri,” akajitetea Gavana Mutai kuhusu madai yanayomkabili ya kumruka mwenzake.