• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Nilidanganywa na Kenya Kwanza, alia Waititu akipigwa na kibaridi nje ya serikali

Nilidanganywa na Kenya Kwanza, alia Waititu akipigwa na kibaridi nje ya serikali

NA MARY WANGARI

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu almaarufu Baba Yao, sasa amefungua moyo kuhusu masaibu yaliyomkumba na yanayozidi kumwandama kisiasa.

Kulingana na mbunge huyo wa zamani katika eneobunge la Embakasi, Nairobi, alihadaiwa na kisha kutemwa na viongozi mashuhuri katika utawala wa sasa unaoongozwa na Rais William Ruto.

Aidha, Bw Waititu aliyewahi kuhudumu kama diwani, ameishutumu serikali ya UDA kwa kumtelekeza hasa kwa kukataa kuingilia kati kuhusu kesi tele zinazomwandama.

Huku akirejelea watu mashuhuri wakiongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Sirisia ambao mashtaka yao yalitupiliwa mbali na afisi ya DPP, Bw Waititu alihoji ni kwa nini bado anaandamwa na kesi chungu nzima.

“Iwapo unatafuta mtu aliyehadaiwa, basi si mwingine ni Waititu. Mimi nilidanganywa,” alisema Bw Waititu katika mahojiano Jumanne yaliyoonekana na Taifa Leo.

“Mmeona kesi zinazoniandama. Nimepokonywa mali hata niliyokuwa nimekusanya kabla ya kujitosa kwenye siasa. Kama wangetaka kunisaidia wangefanya hivyo. Tumeshuhudia DPP akiwaondolea mashtaka watu kadhaa hata akiwemo Naibu Rais.”

Alisema kesi hizo zimemgharimu pakubwa ikiwemo kumkosesha nyadhifa muhimu kama vile uteuzi wake kuwa mwanachama wa Tume ya Mto Nairobi uliositishwa na Jaji wa Mahakama Kuu Hedwig Ongudi mnamo Februari.

“Ukweli ni kuwa nimepigania sana utawala huu. Nimepigania sana serikali hii hata kuliko Rais Ruto mwenyewe. Licha ya juhudi zote hizo, ninahisi nilihadaiwa nikahadaika.”

“Lakini inaweza kuwa vigogo wa Mlima Kenya hawana uwezo kabisa wa kunisaidia ndiposa hawajafanya chochote. Huenda pia ikawa ni njama za kunilemaza kisiasa.”

Bw Waititu alimtahadharisha Dkt Ruto dhidi ya kupotoshwa na viongozi wenye ubinasfi akisema “hali si shwari mashinani.”

“Kuna baadhi ya viongozi ambao kazi yao ni kutoka Bungeni wakielekea makazi yao ya kifahari kama vile Karen na kwingineko pasipo kutangamana kabisa na raia wa kawaida ili waweze kumpa Rais taswira halisi ya hali ilivyo. Wanaendelea kumwambia mambo yako sawa lakini ukweli ni kuwa hali si shwari, wananchi wanateseka, biashara zimefungwa.”

Licha ya masaibu yanayomkabili, mwanasiasa huyo aliyeandikisha historia kwa kuchaguliwa kama kiongozi jijini Nairobi na katika Kaunti ya Kiambu amesema kuwa bado hajakata tamaa kisiasa na atafanya uamuzi kuhusu kugombea baada ya kujadiliana na wapiga kura ifikapo 2027.

  • Tags

You can share this post!

Hakimu aahirisha kesi ya Maina Njenga akilaumu polisi...

Afisa wa polisi aelekeza mtutu wa bunduki mdomoni na...

T L