• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Nilikodishwa tu kusafirisha sukari, mshukiwa ajitetea

Nilikodishwa tu kusafirisha sukari, mshukiwa ajitetea

NA BRIAN OCHARO

MFANYIBIASHARA Chrispus Waithaka anayeshukiwa katika utoroshaji wa magunia 20,000 ya sukari mbaya amesema jukumu lake lilikamilika alipowasilisha mizigo hiyo katika bohari moja mjini Thika.

Katika stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Mombasa, Bw Waithaka alisema alitekeleza jukumu lake la uchukuzi baada ya kampuni yake ya Assets and Cargo Ltd kupewa kandarasi ya kutekeleza shughuli hiyo.

“Jukumu letu lilikuwa tu kusafirisha magunia ya sukari hadi bohari la Vinepack Limited mjini Thika, na kurejesha kontena hizo,” alisema kupitia wakili Kariuki Kamwibua.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, mfanyabiashara huyo alipata kandarasi hiyo mnamo 2022 ili kusafirisha sukari hiyo kutoka bandari ya Mombasa hadi Kiambu.

Mfanyabiashara huyo alisema kampuni yake ilifaulu kusafirisha mizigo hiyo hadi Thika, ambapo ilipokelewa katika yadi kabla ya kuthibitishwa na mashirika ya serikali yakiwemo Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira.

Kulingana na mfanyabiashara huyo, ukaguzi huo wa pamoja ulifanyika na kushuhudiwa na wawakilishi kutoka mashirika ya serikali ambao pia walitia saini hati hizo. Bw Waithaka pia alimweleza Jaji Ann Ong’injo kwamba mkurugenzi wa Vinepack Limited, Peter Mwangi, alithibitisha ipasavyo kwa maandishi kupokelewa kwa mizigo hiyo.

“Baada ya kutekeleza majukumu yetu, jukumu letu sasa ni la kurudisha makontena kwa mmiliki ambayo ni shughuli inayoendelea,” alisema mfanyabiashara huyo.

Alijitetea kuwa alipopewa kandarasi hiyo, alizingatia mahitaji yote kwa hivyo hakutarajia tatizo lolote kutokea.

Bw Waithaka ni kati ya watu wanane walioshtakiwa katika mahakama ya Nairobi kuhusu wizi wa sukari hiyo.

Alishtakiwa pamoja na mkurugenzi mkuu wa KEBS, Bernard Njinu Njiraini ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi na maafisa wengine sita wakuu serikalini kwa kuiba magunia 20,000 ya thamani ya zaidi ya Sh20 milioni.

Mahakama iliambiwa kwamba Bw Njiraini alitumia vibaya ofisi yake kwa kupendekeza kiholela kubadilishwa kwa sukari hiyo kuwa kemikali ya ethanol kupitia mchakato wa kuyeyusha.

Washukiwa wengine ni pamoja na maafisa wa KRA waliosimamishwa kazi Derrick Njeru Kago na Peter Njoroge Mwangi, wafanyabiashara Mohammed Hassan Ali, Abdi Hirsi Yusuf almaarufu Blackie na Pollyanne Njeri Kamau.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Keiyo wakataa naibu chifu asiye mwenyeji

Manchester United wafuzu kucheza michuano ya Klabu Bingwa...

T L