SHANGAZI,
Nina mpenzi ambaye nampenda kwa moyo wangu wote. Tatizo ni kwamba nimezoea kulamba asali nje. Nahisi vibaya kwa kumkosea na ninataka kuacha tabia hiyo. Naomba ushauri wako.
Tabia yako hiyo ni hatari sana. Unaweza kupata magonjwa na kumuambukiza mpenzi wako. Jinsi pekee ya kuacha tabia hiyo ni wewe mwenyewe kuamua kwa kukatiza uhusiano na wanaume wengine. Ukiweka nia hiyo utaweza.
Mpenzi wangu ni mwanamke mfanyabiashara. Amekuwa akigharimia mahitaji yangu yote kwa sababu sina kazi. Sasa anataka nimuoe. Shida ni kwamba hana uwezo wa kupata watoto. Utanishauri vipi?
Uamuzi wako utategemea unachohisi ni muhimu kwako. Kama ni mapenzi na pesa, itabidi ukubali ombi lake. Kama ni watoto, itabidi uachane naye utafute aliye na uwezo wa kukuzalia.
Huu ni mwezi wa sita tangu nilipokosana na mwanamke mpenzi wangu. Juzi alinipigia simu akaomba msamaha na kuniuliza kama ningependa turudiane. Naomba ushauri wako.
Uamuzi wako utategemea iwapo bado unampenda na uko tayari kumsamehe makosa yake. Msamaha huwa si tatizo palipo na mapenzi ya dhati. Ni muhimu ufikirie mambo haya kwanza ndipo ufanye uamuzi unaofaa kuhusu ombi lake.
Nina mpenzi ninayempenda sana na nimekuwa nikimtosheleza kwa mahitaji yake yote. Lakini nimegundua hatosheki, amekuwa akiwagawia asali wanaume wengine wakiwemo marafiki zangu. Nifanyeje?
Nguzo muhimu katika mapenzi ya dhati ni uaminifu. Hali kwamba mpenzi wako anakucheza na wanaume wengine ni thibitisho kuwa hakupendi kwa dhati na anaongozwa na tamaa. Usiendelee kupoteza wakati wako kwake.
>>Usikose safu hii kila Jumatatu hadi Ijumaa saa nne usiku -Mhariri