• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
NMG yatenga siku ya matumizi ya Kiswahili mara moja kila mwezi

NMG yatenga siku ya matumizi ya Kiswahili mara moja kila mwezi

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya habari ya Nation Media Group imeimarisha juhudi zake za kukuza matumizi ya Kiswahili kwa kutenga siku moja kila mwezi kuwa ya matumizi ya lugha hiyo miongoni mwa wafanyikazi wake.

Siku hiyo ya Kiswahili itakuwa inafanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, ambapo wafanyikazi watahitajika kuwasiliana kwa Kiswahili kwenye mazungumzo yao na hata mawasiliano ya barua pepe.

Uzinduzi wa siku ya Kiswahili utafanyika kesho, ambapo wafanyikazi wote wa NMG kuanzia makao makuu jijini Nairobi na afisi zake Mombasa, Kisumu, Nakuru, Nyeri, Eldoret, Meru, Kisii na Kakamega watahitajika kuwasiliana kwa Kiswahili.

Afisa Mkuu wa NMG, Stephen Gitagama alisema hatua hii inalenga kuhamasisha wafanyikazi na Wakenya kwa jumla kujivunia Kiswahili kama lugha inayotambulisha Wakenya na Afrika Mashariki kwa jumla, na pia kufufua ari ya kujivunia utamaduni wa Kiafrika.

Bw Gitagama alisema NMG itaendelea kupiga hatua za kukuza Kiswahili kupitia safu zake kama vile magazeti, runinga, redio na mitandao.

Alieleza kuwa kampuni hiyo inatafuta pia ushirikiano na wadau wengine kama vile taasisi za serikali, vyuo, shule na mashirika mengine ili kukuza na kueneza Kiswahili.

NMG ndiyo inachapisha gazeti pekee la Kiswahili linalochapishwa kila siku nchini la ‘Taifa Leo’. Pia inapeperusha habari na vipindi kwa Kiswahili kupitia runinga ya NTV na tovuti ya taifaleo.nation.co.ke.

You can share this post!

Watumishi wa serikali wasusia mikopo ya magari

Presha Raila amlipe Ruto deni la kisiasa