Na WINNIE ATIENO
Wabunge wa ODM eneo la Pwani wakiongozwa na Bi Mishi Mboko (Likoni), Bi Amina Mnyazi (Malindi), na Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Zamzam Mohammed wameanza kusajili wanachama wa ODM mtandaoni.
Viongozi hao walisema wameanza zoezi hilo baada ya kinara wao wa chama Bw Raila Odinga kuzindua usajili wa wanachama.
Bi Mboko na Bi Mohammed wamewasihi wakazi wa Mombasa kujiandikisha kama wanachama wa ODM ili kuongeza idadi yao na anatumia mtando wa kijamii kuimarisha zoezi hilo la kisiasa.
Akiongea kwenye mtandao wa kijamii, Bi Mboko alisema chama cha ODM kina lengo la kuwakomboa Wakenya kutokana na udhalimu.
“Ninawaomba mjisajili na uwe mwanachama halisi wa ODM. Wale ambao ni wanachama watathmini kama bado ni wanachama wa ODM. Nendeni kwenye mtandao wa chama chetu mjiandikishe. Wingi wetu ni msingi thabiti, tujiandikishe kama wanachama wa ODM ili tuweze kupigana na minyororo ya hali ngumu ya maisha,” alisema Bi Mboko.
Bi Mboko aliwasihi wanawake kujitokeza kwenye siasa ili kubadilisha mkondo wa siasa nchini.
“Hiki ni chama ambacho tunajivunia. Jisalili katika chama chetu, tuweze kupeleke uchumi wa Kenya mbele na tushirikiane kuweza kujenga taifa letu kwa pamoja. Hakuna chama kingine,” alisema Bi Mohammed akimtaja Bw Odinga mtetezi wa wanyonge.
Naye Spika wa Bunge la Kilifi Bw Teddy Mwambire aliwasihi wakazi kujiandikisha kama wanachama wa ODM.
“Ninawasihi viongozi wa ODM wahamasishe umma kuhusu zoezi hili la kitaifa ili tupate ungwaji mkono na umaarufu wa chama. Serikali ya Kenya Kwanza umekumbwa na shutma za ufisadi,” alisema.
Haya yanajiri wiki moja baada ya Kinara wa ODM Bw Raila Odinga kuzindua zoezi la kusaka wanachama nchini.