• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Ole Lenku aenda Uarabuni kuokoa msichana anayeteswa

Ole Lenku aenda Uarabuni kuokoa msichana anayeteswa

Na Stanley Ngotho

GAVANA wa Kajiado Joseph Ole Lenku alilazimika kusafiri hadi milki ya Kiarabu (UAE) ili kumwokoa msichana Maasai ambaye alikuwa akinyanyashwa na mwajiri wake na hata stakabadhi zake kutwaliwa katika taifa hilo linalopatikana Mashariki ya Kati.

Bw Lenku alimwokoa Bi Lillian Rimanto, 23, ambaye alikuwa amekwama Abu Dhabi kwa muda wa miezi minane iliyopita baada ya kuhepa kutoka kwa mwaajiri wake katili mjini Alshamka.

Bi Rimanto alielekea Abu Dhabi mwaka uliopita na akafanya kazi kwa miezi miwili pekee kama mfanyakazi wa nyumbani ila mambo yakaharibika baada ya kunyanyaswa na familia iliyompa ajira.

Alitumia kadi ya simu nyingine kuwasiliana na Wakenya wengine ambao walimpa makao kwa miezi minane baada ya juhudi zake za kurejeshewa stakabadhi zake za usafiri kugonga mwamba.

Humu nchini, jamaa zake kupitia Peninah Soila walimfikia Gavana huyo ambaye alianza kuzungumza na idara husika kisha akasafiri mwenyewe hadi Uarabuni kuomba Bi Rimanto asafiri bila stakabadhi husika.

Isitoshe, Bw Lenku alimnunulia binti huyo tiketi ya ndege kwa kuwa familia yake haikuwa na uwezo wa kupata pesa za kugharimia usafiri wake hadi nyumbani.

“Nilipokuwa mgonjwa na singeweza kufanya kazi, mwaajiri wangu pamoja na familia yake walikuwa wakipika na walihakikisha kuwa chakula chote kinaisha ndipo niwe na njaa hadi nife. Nilinusurika tu kutokana na neema ya mwenyezi mungu,” akasema Bi Rimanto baada ya kuwasili nchini.

You can share this post!

Supkem yashutumu serikali kwa mauaji

Kuzikwa kwa BBI kwageuka pigo kwa Moi Bondeni