• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Onyo kuhusu mafuriko eneo la Ziwa Victoria

Onyo kuhusu mafuriko eneo la Ziwa Victoria

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa maeneo yanayokumbwa na hatari ya mafuriko hasa Nyanza na Budalangi na pia eneo la Magharibi mwa Kenya wameshauriwa wahamie maeneo salama kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo hayo.

Tayari familia kadhaa zimefurushwa makwao kaunti za Kisumu na Migori huku shirika la Msalaba Mwekundu Kenya na wataalamu wa hali ya hewa wakionya kuwa kuna hatari ya mafuriko kutokea kaunti za Homa Bay na Migori.

Katika eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu, mafuriko yameathiri kata ndogo ya Ogenya na zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa Anyuro wamefurushwa makwao.

Kabla ya mvua kuanza mwanzoni mwa mwaka huu, baadhi ya wakazi walikuwa wamerejea katika boma zao lakini wakalazimika kuhama tena wakati maji ya Ziwa Victoria yalianza kuongezeka.

“Tunahofia kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi kufuatia onyo la idara ya utabiri wa hali ya hewa kwamba mafuriko yanaweza kutokea Nyando na maeneo mengine ya nchi,” alisema Chifu wa Kanyagwal, Boniface Nyandeje.

Naibu wa chifu wa Ombaka Kakola, Jacob Ong’udi pia alisema kwamba maafisa wa utawala eneo hilo wanahimiza watu kuhamia maeneo ya miinuko kuepuka kupoteza maisha ya watu, mifugo na mali.

Haya yanajiri huku wakazi wengi wakiomba wafadhili, serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuwasaidia kwa chakula, malazi na makao.

“Mashamba yetu yalifunikwa na maji na hatuna uwezo wa kujikimu,” alisema Judith Ochieng.

Wakazi pia wanaomba misaada ya dawa wakisema visa vya maambukizi ya Malaria na magonjwa yanayosababishwa na maji chafu vimeongezeka.

Katika eneo la Budalangi, kaunti ya Busia, afisa wa Idara ya utabiri wa hewa Benjamin Bahati alisema kwamba afisi yake imewaonya wakazi wa Bunyala wajitayarishe kuhamia maeneo ya miinuko.

“Tumewaonya mapema ili wasipoteze mali yao tena. Itakuwa vyema wakihama mapema,” alisema Bahati.

Kwa wakati huu, baadhi ya nyumba katika eneo la Bunyala Kusini zimesombwa na mafuriko yaliyotokea eneo hilo tangu Machi mwaka jana.

Naibu Kamishna wa Bunyala Kusini, Grace Ouma alisema kwamba nyumba hizo ni za watu waliorejea kutoka kambi za watu ambao waliokolewa katika mafuriko.

Katika eneo la Nyatike, kaunti ya Migori, familia kadhaa zimekosa makao kufuatia mafuriko yanayosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha.

Miongoni mwa vijiji vilivyoathiriwa ni Angugo, Nyora, Modi na Lwanda ambazo zinapatikana karibu na mto Kuja uliovunja kingo zake.

Ripoti za VICTOR RABALLA, GEORGE ODIWUOR SHABAN MAKOKHA na IAN BYRON

You can share this post!

RAMADHAN: Kufunga Ramadhani si mateso bali zawadi kwa...

Waamerika wafurahia utendakazi wa Biden siku 100 baadaye