• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
PANDORA PAPERS: Marais wanavyokwepa ushuru na kuficha mabilioni ughaibuni

PANDORA PAPERS: Marais wanavyokwepa ushuru na kuficha mabilioni ughaibuni

NA FAUSTINE NGILA

MARAIS kadhaa na wakuu wa serikali duniani wametajwa katika ufichuzi wa hivi majuzi wa upelelezi wa jinsi mali ya mabilioni ya hela imefichwa katika visiwa vya ughaibuni ili kukwepa kulipa ushuru.

Ufichuzi huo, Pandora Papers, umeibua hisia kali duniani huku marais wa sasa na wa zamani wa mataifa ya Jordan, Uingereza, Urusi, Czech, Kenya, Azerbaijan, Pakistan, Cyprus, Ukraine na Ecuador wakitajwa kunyima serikali zao mamilioni ya pesa za ushuru.

Ufichuzi wa Pandora ulihusu uchunguzi uliofanywa na zaidi ya wanahabari 600 kutoka vyombo vya habari 140 katika mataifa 117 ambao ni wananchama wa Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari Wapelelezi (ICIJ), ambapo karatasi milioni 11.9 za siri za kifedha kutoka kampuni za huduma za kifedha 14 zilichanganuliwa kote duniani.

Mashirika ya habari ya BBC, Washington Post, New York Times, AFP na The Guardian ambayo ni wanachama wa ICIJ yamefichua kuwa Mfalme Abdullah II wa Jordan anamiliki mali ya thamani ya zaidi ya Sh10 bilioni katika British Virgin Islands.

Tangu aingie uongozini mwaka wa 1999, kiongozi huyo amejizolea mtandao wa nyumba za kifahari 15 nchini Amerika na Uingereza huku mawakili wake wakisema Jordan inaruhusu mabwanyenye kununua mali ughaibuni kisiri .

Ripoti ya uchunguzi huo inafichua kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ameficha mali ya thamani katika kisiwa cha Monaco huku naye Waziri Mkuu wa Czech  Andrej Babis, ambaye anawania kuchaguliwa tena wiki hii, akidinda kuonyesha kampuni iliyonunua nyumba mbili za kifahari za Sh1.3 bilioni kusini mwa Ufaransa na mali nyingine ya Sh4 bilioni Uingereza.

Washiriki wakaribu wa Waziri Mkuu wa Pakistan wakimewa mawaziri na familia zao wametajwa kumiliki mali fiche ka kampuni za mabilioni ya fedha.

Nayo kampuni ya uansheria ya Rais Nicos Anastasiades wa Cyprus iliwasilisha wamiliki bandia ili kuficha mmiliki halisi wa mtandao wa kampuni kadhaa katika visiwa vya ughaibuni, lakini kampuni hiyo imekana kuhusika, ripoti hiyo imesema.

Imeibuka pia kuwa Rais wa Ecuador Guillermo Lasso ambaye alifanya kazi kwa benki kwa miaka mingi, alibatilisha wakfu wa Panama uliotuma hela kila mwezi kwa familia yake na kampuni iliyoko South Dakota, Amerika.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair na mkewe waliokoa Sh46 milioni za ushuru waliponunua ofisi moja jijini London huku wakinunu kampuni ya ughaibuni iliyomiliki jumba lenye ofisi hiyo.

Cha kushangaza ni jinsi familia ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ilinunua nyumba 17 za kifahari, ikiwemo moja ya thamani ya Sh3.4 bilioni jijini London iliyopewa mwanawe rais huyo ambaye ana miaka 11, Heydar Aliyev.

Akihojiwa na BBC, Bw Fergus Shiel kutoka ICIJ alisema kuwa hakujawahi kutokea ufichuzi mkubwa kuliko wa sasa na inaonyesha jinsi kampuni za ughaibuni zinaweza kusaidia watu kuficha hela walizopata kwa mbinu isiyostahili au kukwepa kulipa ushuru.

“Wanatumia akaunti hizi za visiwani na kampuni kununua mali ya thamani ya mabilioni ya pesa katika mataifa mengine, na pia kutajirisha familia zo wenye, huku wananchi wakiendelea kuumia,” alisema.

Kulingana na Maira Martini, mwansera katika Transparency International, ufichuzi huo umeonyesha jinsi kampuni za visiwani zinachochea kuenea kwa ufisadi na wizi wa pesa huku vikizuia wananchi kutendewa haki.

“Mfumo huu wa biashara haufai kuruhusiwa kuendelea,” aliambia AFP.

Pandora Papers ndiyo ripoti ya hivi majuzi katika msururu wa upelelezi unaoongozwa na ICIJ ambapo stakabadhi za siri za kifedha hufichuliwa kwa umma kuanzia LuxLeaks hapo 2014, Panama Papers ya 2016, Paradise Papers ya 2017 nq FinCen files ya 2020.

 

 

You can share this post!

Idara yajiandaa kushughulikia kesi tele za uchaguzi 2022

Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka