• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Pasta aliyekwama hotelini aomba asaidiwe na Sh370,000

Pasta aliyekwama hotelini aomba asaidiwe na Sh370,000

NA TITUS OMINDE

PASTA mwenye umri wa miaka 39 na wenzake wawili, wanaomba wasamaria wema kuwaokoa, baada ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa kufanya maombi kwa siku 41 katika hoteli moja mjini Eldoret, na kushindwa kulipa bili ya zaidi ya Sh371,000.

Pasta Alex Munyoki na wenzake walipiga kambi katika hoteli ya Goshen ili kuombea nchi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Watatu hao wameshtakiwa katika Mahakama ya Eldoret kwa kupokea huduma kwa njia ya uongo.

Kulingana na pasta huyo, mshirika wake kutoka Amerika alikuwa ameahidi kugharimia bili wakati wa maombi hayo lakini baadaye alikataa kupokea simu zake na kulazimisha wasimamizi wa hoteli kuwazuilia.

Kisa hicho kilifanyika Machi 28, 2023 wakati pasta huyo alikodisha vyumba vitatu vya kufanya maombi na kufunga.

Jumanne Desemba 5, 2023 kesi ilipotajwa mbele ya Mahakama ya Eldoret, watatu hao walishukuru usimamizi wa hoteli hiyo kwa kuwa wavumilivu kwa siku 41, huku wakitafuta namna ya kulipa hela hizo.

“Mimi ni mchungaji ninayetambulika sana Kaunti ya Kitui, sitaki jina langu kuchafuliwa kwa kukosa kulipa bili. Ninafanya mazungumzo na hoteli kuondoa kesi hii huku nikiomba wasamaria wema kunisaidia pamoja na aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Mike Sonko,” alisema Pasta Munyoki.

Pasta Munyoki alisema maombi hayo yalikuwa ya nchi na akasikitika mtu aliyestahili kulipa gharama hiyo aliingia mitini huku akielezea nia yake ya kutaka kulipa deni hilo.

Pasta Munyoki, Bw Gilbert Muzami Mukisa, 32 na Lilian Namangasa Walukana, walishtakiwa kwa kupokea huduma za hoteli kwa njia ya uongo kinyume na sheria. Watatu hao walikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi, Bw Richard Odenyo na kusema wana imani Mungu atatuma malaika kuwaokoa.

Katika taarifa yake mahakamani, Bw Munyoki alidai, “Mungu alimwambia kwenye ndoto kuhusu kuja kwa Yesu” na akawatafuta marafiki wawili ambao waliandamana naye kwenye maombi.

Wakati wa kukamatwa kwake, Bw Munyoki mkazi wa Kaunti ya Kitui, ambaye alilelewa katika kanisa la Redeemed Gospel, aliambia maafisa wa upelelezi kwamba Mungu alimwelekeza kwenye hoteli hiyo.

Pia, walitumia chumba kimoja na mwenzake Gilbert wakilala kwenye kitanda kimoja huku mwenzao wa kike akitumia chumba kingine kufanikisha maombi ya mchana na usiku.

Alidai alikutana na mfadhili kutoka Amerika kwa jina Rooney, Kaunti ya Machakos, na akaahidi kulipa gharama yote ila baadaye hakupatikana kwa simu.

Hakimu Odenyo, aliachilia washtakiwa kwa dhamana ya Sh80,000 au pesa taslimu ya Sh60,000 kila mmoja.

Kesi hiyo itaendelea Desemba 6.

  • Tags

You can share this post!

Makali ya njaa Mathare yanavyosukuma mabinti wachanga...

Hapa vitenge na jezi tu: Sababu za Mkuu wa Utumishi wa Umma...

T L