• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
Polisi mpakani wapepeta corona kwa hongo ya Sh2,000

Polisi mpakani wapepeta corona kwa hongo ya Sh2,000

SIAGO CECE na ANTHONY KITIMO

UFISADI miongoni mwa baadhi ya maafisa wa serikali katika mpaka wa Kenya na Tanzania, umezidi kuwaweka wananchi katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Katika kipindi cha chini ya wiki moja baada ya maafisa wanaosimamia mpaka ulio Lungalunga, Kaunti ya Kwale kulaumiwa kwa utepetevu uliosababisha washukiwa wa ugaidi kuingia nchini wakiwa na silaha, Taifa Leo imebaini kuwa maafisa katika mpaka huo huruhusu wasafiri wasio na stakabadhi za kutoambukizwa Covid-19 wavuke mpaka huo.

Imebainika kuwa maafisa wa afya, uhamiaji, polisi na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma huwa wanashirikiana kuruhusu wasafiri wasio na vyeti vya kuonyesha hawana maambukizi ya corona wavuke mpaka baada ya kulipa hongo ya hadi Sh2,000.

Mahojiano tuliyofanyia baadhi ya wasafiri yalithibitisha kuwa hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu sasa.

“Jumapili iliyopita, nilivuka mpaka nikaenda hadi Tanzania bila cheti baada ya kumlipa kondakta wa basi Sh2,000 zaidi ya nauli ya kawaida. Alitutengenezea stakabadhi zetu hata bila kushuka katika basi. Nililazimika kufanya hivyo kwa sababu nilikuwa na safari ya dharura inayohitaji nipate chanjo, na niliingia Tanzania nikapewa chanjo niliyotaka,” akasema mmoja wa abiria.

Alifichua kuwa, kutokana na vile baadhi ya mataifa hasa ya Ulaya hayatambui chanjo ya AstraZeneca, kuna Wakenya ambao huelekea Tanzania kupokea chanjo ya Johnson & Johnson kabla wasafiri kwenda ng’ambo.

Mbali na hayo, chanjo ya AstraZeneca haitolewi cheti hadi mtu adungwe mara mbili, na chanjo ya pili hutolewa baada ya wiki nane.

“Niliamua niende Tanzania kwa sababu huko ndipo ningeweza kupata chanjo ya Johnson & Johnson kisha cheti chatolewa papo hapo, tofauti na Kenya ambapo hata ukishapata chanjo ya AstraZeneca, hutapata cheti hadi upate chanjo ya pili itakayokuja baada ya wiki nane,” akaeleza.

Maafisa wa usalama katika Kaunti ya Kwale walithibitisha kumekuwa na madai ya watu kuvuka ndani na nje ya mpaka wa Kenya na Tanzania bila vyeti vya kuthibitisha kama wanaugua Covid-19 au la.

Kamishna wa Kwale, Bw Joseph Kanyiri ambaye anasimamia vikosi vya usalama katika kaunti hiyo alisema iwapo upelelezi wao utabainisha kuwa madai hayo ni ya kweli, itakuwa ni masikitiko kwani itamaanisha wananchi wengi wamewekwa katika hatari ya maambukizi bila kujua.

“Hili ni jambo ambalo tutahitaji kuchunguza. Tuna maafisa wa afya wa mpakani ambao husimamia masuala ya Covid-19 na magonjwa mengine, idara ya uhamiaji inayochunguza jinsi watu wanavyoingia na kutoka nchini, na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) inayothibitisha malipo ya bidhaa zinazovukishwa mpakani. Hili ni jambo ambalo tutachunguza ili tujue ni idara gani hasa inayohusika katika kufanikisha hayo,” akasema Bw Kanyiri.

Hata hivyo, aliwatetea maafisa wa Kenya na kusema kama madai hayo ni ya kweli basi kuna uwezekano mkubwa matukio hayo yanafanywa kwa ushirikiano na wale walio upande wa Tanzania.

Wakati huo huo, Bw Kanyiri alisema usalama umeimarishwa mpakani na vikosi tofauti vya usalama ili kuzuia aina yoyote ya wahalifu kuingia nchini.Hii ni baada ya washukiwa wawili wa ugaidi kukamatwa wiki iliyopita, wakisemekana walikuwa wamesafiri kutoka Tanzania.

You can share this post!

Waislamu walaani MUHURI kuajiri ‘mtetezi wa...

Wafuasi 13 wa UDA washtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni za...