• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Polisi wasaka mwanamke mshukiwa wa mauaji aliyenaswa akiruka ukuta wa seng’eng’e

Polisi wasaka mwanamke mshukiwa wa mauaji aliyenaswa akiruka ukuta wa seng’eng’e

NA LABAAN SHABAAN

PICHA za mwanamke mshukiwa wa mauaji ya kikatili ya mwanamume polisi waliyemtambua kama Dkt Eric Maigo Septemba 15 2023 alfajiri zimeanikwa mitandaoni huku Idara ya Ujasusi wa Jinai (DCI) ikiwaomba Wakenya watoe ripoti kuhusu aliko atiwe mbaroni.

Picha hizo zilizonaswa na kamera za usalama za CCTV zinaonyesha mwanamke akiruka ukuta wenye seng’eng’e baada ya ‘kutekeleza mauaji’ usiku wa manane katika makazi ya Bw Maigo, eneo la Woodley Annex – Upper jijini Nairobi.

“Mshukiwa aliyenaswa na kamera akiondoka makazi ya mwathiriwa anaaminiwa kuhusika na mauaji mabaya zaidi kabla ya kutoroka kupitia mlango wa nyuma,” DCI ilisema kwenye mtandao wa X ikiongeza kuwa visu viwili vyenye damu vinavyoaminiwa kuwa silaha za mauaji vilipatikana katika eneo la jinai.

Huku wakisema wanajizatiti kumnasa mshukiwa, makachero hao wanaomba wananchi wawasaidie kutoa habari zitakazotoa mwelekeo kumnasa haraka iwezekanavyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa Hospitali ya Nairobi Eric Maigo aliuliwa kwa kudungwa kisu mara 25 kama ilivyothibitishwa na upasuaji wa mwili katika hifadhi ya maiti ya Lee.

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alisema muuaji alimkalia mwathiriwa tumboni na kumjeruhi vibaya hadi kumuua.

Kabla ya kukutana na mauti yake, Dkt Maigo alikuwa katika kilabu maarufu mkabala na Barabara ya Ngong ambapo alikutana na watu kadhaa wakiwemo wanawake watatu ambao wanasadikiwa kuhusika na kifo hicho.

Katika harakati za ujasusi kutegua kitendawili cha mauaji, makachero walitembelea kilabu hicho kuwatambua waliotangamana naye kutumia kamera za usalama eneo hilo.

Mmoja wa washukiwa Bi Cynthia Lusega Andalo alikamatwa na kufikishwa mahakamani Jumatatu adhuhuri na polisi wakapewa muda wa siku tano kumzuia kama njia ya kuchunguza tukio la kifo hicho.

Hospitali ya Nairobi inamtaja Bw Eric kuwa mfanyakazi aliyejitolea kwa ufanisi wa huduma za kituo hicho cha afya.

  • Tags

You can share this post!

Mlima Kenya walia kupanda kwa gharama ya maisha licha ya...

Kilio Man-U, Arsenal ikipiga sherehe Uefa

T L