• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Pwani yazama El Nino ikitishia kunyima hoteli mahanjam ya watalii Krismasi

Pwani yazama El Nino ikitishia kunyima hoteli mahanjam ya watalii Krismasi

Na WAANDISHI WETU

“Nimepoteza mbuzi 15 na ng’ombe wanane kutokana na mafuriko. Ilinibidi kuondoka nyumbani kwangu kuokoa maisha yangu na wajukuu wangu sita,” anasema Fathma Sawen, 81, mwathirika wa mafuriko kutoka kijiji cha Bandi huko Tana Delta.

Ajuza, Sawen anasema ana bahati ya kuwa hai pamoja na wajukuu wake ambao pia alifanikiwa kuwaokoa mbuzi wawili kutoka kwa mafuriko hayo wakati wakitoroka kutoka kwa janga hilo Jumapili jioni.

“Siwezi sema nimepata hasara ya aina gani. Lakini nina furaha kuwa hai,” anaongeza Bi Sawen, mjane ambaye amekuwa akiishi na wajukuu wake sita ambao walikuwa mayatima zaidi ya miaka mitano iliyopita.

“Mimi ndiye mama na baba yao. Mkubwa ana umri wa miaka 15 wakati mdogo ana umri wa miaka 15,” alisema Bi Sawen.

Yeye ni miongoni mwa watu 600 ambao wamekita kambi katika Mji wa Minjila kuanzia sasa.

Vijiji vya Tara na Ongonyo kwa upande mwingine vina jumla ya zaidi ya familia 800 zinazotafuta uhifadhi katika Kijiji cha Oda.

Uhamaji mkubwa kutoka kwa vijiji vinavyokabiliwa na mafuriko unaendelea katika eneo la Pwani huku kukiwa na tahadhari ya hali mbaya zaidi.

Wakazi wanakimbia makazi yao kutafuta hifadhi kwenye maeneo yaliyoinuka, mamia yao kwa sasa wanaelekea kupiga kambi kando ya barabara kuu ya Malindi-Garissa.

Hofu yao kuu ni kukosa huduma za afya pamoja na msaada wa kibinadamu.

Makumi ya nyumba zimesongwa na mafuriko na maji yanapoendelea kuongezeka, kukaa sio chaguo kwa hivyo kukimbilia kuhama.

“Mto tayari umejaa maji na kumwagika, kila siku naamka kijijini kwangu naona maji yakisogea karibu na nyumba yangu na hiyo ni kengele,” alisema Mohammed Abdi, mkazi wa kijiji cha Bandi.

Kulingana na Bw Abdi, dalili zote zinaonyesha kwamba mgogoro wakati huu hautalinganishwa na wowote, na bado haujadhihirika.

Iwapo mvua itaendelea kwa kasi hiyo hiyo, zaidi ya vijiji 30 katika Delta ya Tana vitazama.

“Kwa kawaida wakati wa mafuriko, vijiji vinakatika au kusombwa lakini mambo yalivyo kwa sasa, maji ni mengi ukilinganisha na mafuriko ya kawaida, hatutakuwa na vijiji vingi vinavyonusurika kwa kile kinachokuja,” alisema.

Katika kijiji cha Sogal, zaidi ya vijiji 500 vinahamia Oda.

Ni safari ndefu ambayo itawachukua siku mbili, kwani inawalazimu kupita kwenye maji ya mafuriko hadi kijiji kinachofuata.

“Tutapumzika katikati na kuendelea na safari kesho, barabara imejaa maji na ni hatari kwa nyoka na nge,” alisema Abdulahi Hussein.

Mamia ya wengine wanahama kutoka vijiji vya Ongonyo na Tara hadi maeneo salama.

Gavana Abdulswamad Nassir, anaendeleza juhudi zake za kusadia waathiriwa wa mafuriko.

Baadhi ya majumba katika eneo la Bamburi, Kiembeni na Utange bado zimezingirwa na kuingiwa maji.

“Mahandisi wanaendeleza juhudi za kuchota maji katika sehemu ambazo zimezingirwa na maji kwa kutumia pampu. Ninawarai wakazi kutoogelea kwenye mafuriko ni hatari,” alisema Gavana Nassir.

Kwa jumla watu 11 wameapa dunia huku wengine familia 10,000 kuathirika na janga la mafuriko eneo la Pwani kutokana na mvua iliyonyesha mfululizo siku tano zilizopita.

Mshirikishi wa eneo la Pwani, Bi Rhoda Onyancha alisema kaunti zilizoathirika pakubwa ni Mombasa, familia 3892, na Tana River 5136.

Na Mkamburi Mwawasi, Cece Siago,Winnie Atieno na Stephen Oduor

  • Tags

You can share this post!

KRA yaelekeza mkono wake kwa mabilioni ya mawakili kwenye...

Mwalimu akatwa na mbawa za helikopta Garissa na kufariki

T L