• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Raila aonya siasa isiingiziwe usimamizi wa Mumias

Raila aonya siasa isiingiziwe usimamizi wa Mumias

NA SHABAN MAKOKHA

KINARA wa Azimio Raila Odinga amewataka viongozi wasiingize siasa kwenye usimamizi wa Kiwanda cha Mumias akionyesha imani kuwa Sarrai Group, mwekezaji anayesimamia kiwanda hicho, atafaulu kukifufua.

Bw Odinga alisema kuwa hatua ya viongozi kuendelea kuingiza siasa kwenye usimamizi wa kiwanda hicho kumekuwa kukiwaathiri sana wakulima.

Masaibu ya Kiwanda cha Mumias yalianza 2012/13 kilipoanza kupata hasara kabla ya kuporomoka kabisa 2018 kutokana na hasara ya Sh39.44 bilioni.

Akizungumza katika eneobunge la Matungu mnamo Jumamosi, Desemba 2, 2023 Bw Odinga alisema Sarrai Group inastahili kupewa muda wa kufufua kiwanda hicho.

“Mimi ni mhandisi na nimetembelea kiwanda hicho kuangazia juhudi za kukifufua. Kama mhandisi, naweza kuwaambia kuwa kuna mipango ya kueleweka kufufua Mumias,” akasema Bw Odinga.

“Tupunguze kelele ambazo tumekuwa tukipiga kuhusu Mumias na badala yake tumpe mwekezaji mpya muda wa kuwajibika,” akaongeza huku akisema kuwa iwapo Sarrai atapokonywa mkataba aliopewa wa miaka 20, huenda akarejea kortini na kuzamisha juhudi za kufufua kiwanda hicho.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alionya kuwa jinsi ambavyo viongozi kutoka Magharibi wanaendelea kutofautiana kuhusu Mumias, ndivyo pia wanazidi kumhofisha mwekezaji na hata wengine ambao wangekuwa na nia ya kukifufua kiwanda hicho.

Wiki iliyopita, Rais William Ruto aliamrisha kamati ya wataalamu iangazie madeni ya Mumias ya Sh33 bilioni kisha itoe mwongozo wa jinsi kinaweza kurejelea shughuli zake.

Rais alikutana na viongozi wa kutoka Kaunti ya Kakamega wakiongozwa na Gavana Fernandes Barasa ambapo walijadili jinsi ambavyo kiwanda hicho kinaweza kurejelea shughuli zake.

Bw Barasa alinukuliwa akisema mkutano na Rais ulikuwa wa kuwanufaisha wakulima wa miwa.

Viongozi kutoka Magharibi nao walisema kuwa Rais Ruto anastahili kutimiza ahadi aliyotoa ya kukifufua kiwanda hicho.

Waziri wa zamani wa michezo Rashid Echesa alimtaka Bw Barasa pamoja na viongozi wenzake, wakumbushe Rais kuwa Sarrai hawezi kuamsha Mumias na anastahili kumleta mwekezaji mwenye uwezo wa kufaulisha mchakato wa kufufua kiwanda hicho.

“Siamini kuwa Sarrai ina uwezo wa kufufua Mumias. Tunahitaji mwekezaji mpya wa kufufua Mumias ili wakulima nao waendelee kunufaika,” akasema Bw Echesa.

 

  • Tags

You can share this post!

Vidosho Akorino walionengulia walevi viuno wawaka moto

Besigye amshambulia Rais Museveni kwa kukwamilia uongozini

T L