• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Raila: Utawala wa kimikoa ufutiliwe mbali

Raila: Utawala wa kimikoa ufutiliwe mbali

NA WYCLIFFE NYABERI

KINARA wa ODM Raila Odinga amesema utawala wa zamani wa kimikoa maarufu kama Provincial Administration unafaa kufutiliwa mbali mara moja.

Bw Odinga amedokeza kwamba utawala huo ulimalizwa na Katiba ya mwaka 2010 na inasikitisha kuwa bado ungalipo.

Ametaka nyadhifa kama makamishina wa kaunti na waratibu wa serikali wa kanda mbalimbali kuondolewa akidai zinahujumu serikali za ugatuzi ambazo zilibuniwa na Katiba ya sasa.

Akiongea mnamo Desemba 3, 2023, alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa mbunge wa zamani wa Mugirango Magharibi Benson Kegoro katika Kaunti ya Nyamira, kiongozi huyo wa upinzani alisema Katiba ya 2010 ilibuni nafasi za magavana, ambao huchaguliwa na wananchi.

Hivyo, kulingana na Odinga, magavana wanafaa kupewa nguvu zaidi kutekeleza majukumu ya kiserikali.

“Katiba ya 2010 ilileta ugatuzi na ni lazima tutetee mfumo wa kaunti kwa udi na uvumba. Magavana ndio Maafisa Wakuu Watendaji wa Kaunti na hivyo wanafaa kupewa nguvu kufanya kazi rasmi za kiserikali. Lakini inasikitisha kuona watu kama makamishina wa kaunti na waratibu wa serikali wa maeneo, ambao ni wa kuteuliwa tu wakifanya maamuzi kama ya kuagiza mali ya watu na nyumba zao kubomolewa. Hilo halifai,” Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema katika eneobunge la Borabu ambapo mazishi ya marehemu Kegoro yalifanyika.

Bw Odinga hakusita kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kile alisema imeshindwa kuwatimizia Wakenya ahadi nyingi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

“Walikuwa wakisema mama mboga, mtu wa jua kali, bodaboda na kadhalika. Lakini sasa lugha yao imebadilika. Ahadi zao zilikuwa hewa tu. Walisema watawainua Wakenya kutoka chini kwenda juu, lakini yale tunayoshuhudia ni kinyume. Gharama ya maisha imepanda. Viwango vya ushuru vimeongezwa maradufu. Hakuna kusema tena punda amechoka bali punda ameanguka,” akasema Odinga huku akiibua kicheko kutoka kwa waombolezaji waliokuja kumpa buriani ya mwisho mwanasiasa huyo mkongwe.

Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua pia alihudhuria mazishi hayo ya mwendazake Kegoro.

Karua alikuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, 2022.

Naye, aliwataka viongozi wote waliochaguliwa kufanya majukumu yao ipasavyo.

Alisisitiza kuwa watazidi kushinikiza serikali ili itafute mbinu za kushusha gharama ya maisha.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi wa vyuo wanavyomezea mate mijibaba

Vidosho Akorino walionengulia walevi viuno wawaka moto

T L