NA COLLINS OMULLO
RAIS William Ruto anaonekana kutelekeza baadhi ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita huku mahasla waliompigia kura wakilemewa na gharama ya juu ya maisha.
Akijipigia debe wakati huo, Dkt Ruto alikosoa baadhi ya sera za mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akidai ndizo zimezamisha uchumi wa nchi.
Hata hivyo, mambo yalionekana kubadilika na kuchukua mkondo tofauti pindi tu Dkt Ruto alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya.
Akiwa madarakani kwa muda wa miezi minane tu, Rais Ruto sasa anaonekana kulegeza kamba na kusahau ahadi alizotoa hapo awali. Ili kukabiliana na gharama ya juu ya maisha, Rais alizundua manifesto ya ‘Bottom Up’ aliyodai ingerekebisha makosa ya utawala wa Bw Kenyatta. Kwenye manifesto yake, Rais alitoa ahadi kadhaa akidai angezitekeleza ndani ya siku 100 madarakani, jambo ambalo hajalitimiza.
Akiwa madarakani, alitimiza haraka ahadi ya kuwateua mara moja majaji sita ambao mtangulizi wake alikataa kuwaapisha. Kadhalika, aliongeza mgao wa bajeti kwa Idara ya Mahakama kwa kuitengea idara hiyo Sh3 bilioni kila mwaka.
Rais pia alitia saini Amri ya Utendaji inayoipa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) uhuru wa kifedha. Haya yote aliyafanya ili kuonekana mchapakazi na kuenda kinyume na sera za Bw Kenyatta. Hata hivyo, Rais Ruto aliendelea kuwafinyilia kabisa mahasla kupitia Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2023. Kwenye mswada huo, serikali inalenga kutoza kodi kubwa zaidi – ikiwa ni pamoja na asilimia 16, kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta.
Kwa sasa, Rais anatetea sera ya kodi ya utawala wake, akisema kodi hizo mpya zitaongeza pato la taifa kutoka asilimia 14 hadi asilimia 16.
Kadhalika, Rais Ruto ameahidi mara sio moja kupunguza bei ya mbolea ili kuwawezesha wakulima kuongeza mavuno yao. Pia, aliahidi kuwaajiri walimu wasiopungua 35,000 kama hatua nyingine ya kimaendeleo.
“Nimelazimika kufanya maamuzi magumu tangu niingie afisini, kama vile kusimamisha ruzuku kadhaa zilizokuwa zikitolewa kila mara na serikali ya Bw Kenyatta. Hii ilifanya uchumi wa nchi kuzama zaidi,” Dkt Ruto alisema akitetea uamuzi wake wa kufutilia mbali ruzuku.
Kadhalika, Rais Ruto aliahidi kuwa serikali yake ingeunda nafasi za ajira kwa mahasla, jambo ambalo hajalitimiza. Baada ya kuapishwa, alitupilia mbali mpango wa Kazi Mtaani ulioundwa na mtangulizi wake kuwasaidia vijana kujikwamua kutokana na janga la corona.
Badala yake, alisema vijana waingie katika miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama ya chini. Akitetea hatua yake ya kuwateua mawaziri wasaidizi 50, Rais Ruto alidai serikali yake inahitaji watu wengi ambao wangemsaidia kutimiza ahadi zake.
“Ajenda yangu kwa Kenya inahitaji watu wengi na akili zaidi, ndiyo maana ninahitaji mawaziri wasaidizi wengi. Pia, nataka serikali yangu iwajibike na ndiyo maana napinga kushirikiana na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga,” akasema Rais.
Hata hivyo, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana, Jackson Ole Sapit walikashifu uteuzi wa rais wakidai kuwa unaendeleza ukabila.
“Kuna ukabila na urafiki wa wazi hasa kuhusiana na uteuzi wa umma… Hili halikubaliki. Acheni taasisi na afisi zote za serikali zisiwe na upendeleo na zisiwe na ushawishi wa kisiasa tu na kuwahudumia Wakenya wote bila upendeleo,” akasema Askofu Sapit.