• Nairobi
  • Last Updated February 23rd, 2024 12:48 PM
Rais Ruto aongoza mkutano wa kundi la Wabunge na Maseneta wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi

Rais Ruto aongoza mkutano wa kundi la Wabunge na Maseneta wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi

NA CHARLES WASONGA 

RAIS William Ruto leo Jumanne, Mei 23, 2023, ameongoza mkutano wa Kundi la Wabunge wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi.

Mkutano huo umejiri saa chache kabla ya Bunge la Seneti kurejelea vikao vyake vya kawaida kuanzia saa nane na nusu baada ya likizo fupi ya maseneta.

Duru kutoka mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua zimesema kuwa miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika mkutano huo ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kaunti zote nchini.

“Mkutano huo pia umejadili mipango ya serikali ya kushughulikia kero ya uhaba wa ajira miongoni mwa vijana nchini. Rais amewajuza wabunge na maseneta wa Kenya Kwanza kuhusu mipango ya serikali yake ya kuanzisha vituo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika kila mojawapo ya wadi zote 1,450 nchini ili kubuni ajira za kidijitali kwa vijana wetu,” amesema mbunge ambaye aliomba tulibane jina lake.

Rais amesema kuwa amekubaliana na magavana kuhusu wazo la kuanzishwa kwa maeneo ya kilimo na viwanda katika kila kaunti na masoko katika kila mojawapo ya kaunti ndogo.

“Mpango huu ambao umetajwa katika manifesto ya Kenya Kwanza ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuchochea ukuaji wa kiuchumi na kupunguza gharama ya maisha,” akasema mbunge huyo kutoka eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Rais Ruto pia ametumia mkutano huo kuendelea kuwarai wabunge wa Kenya Kwanza wapitishe Mswada wa Fedha wa 2023 ambao serikali inalenga kutumia kuimarisha ukusanyaji wa ushuru ili kufadhili bajeti yake ya kwanza ya Sh3.6 trilioni.

Hii ni licha ya kwamba mswada huo umepingwa na viongozi wa upinzani pamoja na Wakenya wa tabaka mbalimbali kwa kuwa unalenga kuwaongezea wananchi mzigo wa ushuru.

Wakati huu wadau mbalimbali na Wakenya kwa ujumla wanatoa maoni na mapendekezo yao kuhusu mswada huo katika vikao vya umma vinavyoongozwa na Kamati ya Bunge kuhusu Fedha. Kamati hiyo yenye wanachama 17 inaongozwa na Mbunge wa Molo, Kuria Kimani.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala kutetemesha kwenye riadha za Diamond League

Maafisa wa Kamati ya Makabidhiano ya Afisi ya Gavana...

T L