• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Ruto alituenjoi kuhusu mapato ya Tsavo, asema Seneta wa Taita Taveta

Ruto alituenjoi kuhusu mapato ya Tsavo, asema Seneta wa Taita Taveta

NA LUCY MKANYIKA

SENETA wa Taita Taveta Jones Mwaruma ametofautiana na Rais William Ruto kuhusu ugavi wa mapato ya Hifadhi ya Tsavo, akisema kuwa ahadi ya asilimia 50 ya mapato kwa kaunti haitawezekana.

Seneta Mwaruma alisema matamshi ya Rais yanapotosha wananchi, akifafanua kwamba Tsavo haina mapato ya kutosha ya kugawanywa kati ya serikali ya kitaifa na ile ya kaunti.

Haya yanajiri huku viongozi wa eneo hilo wakimpongeza Rais kwa ahadi hiyo.

Matamshi ya Bw Mwaruma yanamfanya kuwa kama msaliti wa kaunti hiyo, ambapo wananchi wamekuwa wakililia serikali kutekeleza mpango huo ili wanufaike kutoka kwa mbuga hiyo ambayo imekuwa donda sugu kwa wenyeji.

Bw Mwaruma, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais na serikali yake, alimlaumu Dkt Ruto kwa kuendelea kupiga kampeni na kutoa ahadi kwa wakazi zisizotekelezwa.

Alidai kuwa serikali imepuuzilia mbali eneo hilo na kulitumia kama chombo cha kisiasa, huku akiwataka wakazi kushinikiza uwajibikaji na maendeleo kutoka kwa utawala wa Dkt Ruto.

Kuhusu Tsavo, Bw Mwaruma alisema kuwa hifadhi hiyo, haitoi mapato ya kutosha ya kugawanywa kati ya serikali ya kitaifa na ya kaunti, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa kaunti kupata fedha zozote.

“Rais hana dhamira njema na ndio maana nilisema sitahudhuria mikutano yake wakati wa ziara zake za eneo hili. Anajua vyema kuwa mbuga ya Tsavo haitoi pesa za kutosha kwa hivyo atatoa wapi asilimia 50 kuwapa wenyeji?” Bw Mwaruma aliuliza.

Wakati wa ziara yake katika kaunti hiyo mwezi Julai, Rais aliahidi kuwa kaunti itapata angalau asilimia 50 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwa hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Seneta Mwaruma, alidai kuwa Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS), ambalo linasimamia hifadhi hiyo, limekuwa likitegemea mgao wa serikali kuu ili kutekeleza majukumu yake.

Alitaja ripoti ya kamati ya bunge iliyofichua kuwa KWS haikuweza kupata mapato ya kutosha kugharamia shughuli zake.

Seneta huyo alimtaka Rais kusema ukweli kuhusu mapato ya hifadhi hiyo kwa wakazi na jinsi anavyokusudia kutekeleza mpango wa ugavi wa mapato hayo.

“Tunataka Rais atuambie ukweli na atupe maendeleo,” alisema.

Seneta Mwaruma, ambaye ni kiongozi wa chama cha ODM na muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja, aliahidi kuendelea kupigania haki na maslahi ya wenyeji wa eneo hilo.

Alikosoa wenzake wa eneo hilo ambao wameahidi kufanya kazi na Rais.

“Katiba inatupa haki ya kupata maendeleo bila kujali mwelekeo wetu wa kisiasa. Mimi kama seneta niko ndani ya serikali lakini katika kitengo cha kutunga sheria. Kwa hivyo wabunge wa upinzani wakisema kuwa watafanya kazi na serikali wamepoteza mwelekeo,” alisema.

Kinyume na matamshi ya seneta, viongozi wengine katika kaunti hiyo wamekumbatia tangazo la Rais.

Gavana Andrew Mwadime aliitaka serikali ya kitaifa kutuma mgao wa kwanza mwezi ujao ili kuboresha maendeleo ya eneo hilo.

Aidha, Kamati ya Bunge ya Utalii na Wanyamapori inayoongozwa na Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki ilisema imeanza kuzingatia pendekezo la kutunga sheria ili kuwezesha mpango huo.

Hata hivyo, Bw Mbiuki alionya serikali ya kaunti hiyo dhidi ya kuwa na matarajio yanayopita kiasi kuhusu mpango huo akisema kuwa hifadhi hiyo haitoi mapato ya kutosha kugawanywa kati yao na serikali ya kitaifa.

Hivi majuzi, mpango huo vilevile ulipingwa na kaunti zingine zinazopakana na hifadhi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mwalimu akatwa na mbawa za helikopta Garissa na kufariki

Hakimu aahirisha kesi ya Maina Njenga akilaumu polisi...

T L