• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:55 PM
Sakata ya Kemsa: Terry Ramadhani adai waziri Nakhumicha alijaribu kumshawishi

Sakata ya Kemsa: Terry Ramadhani adai waziri Nakhumicha alijaribu kumshawishi

NA MARY WANGARI

AFISA Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) aliyesimamishwa kazi amefichua jinsi Waziri wa Afya alivyojaribu kumshawishi kukubali neti za kuzuia mbu zilizotibiwa bila malipo kutoka kwa kampuni moja.

Akijibu maswali Jumanne mbele ya Seneti kuhusu sakata ya Sh3.7 bilioni ya vyandarua vya kujikinga na malaria, Bi Terry Ramadhani, aliwasilisha barua aliyodai ilitumwa na waziri Susan Nakhumicha mnamo Aprili 23, 2023.

Katika barua hiyo iliyotiwa mhuri wa Wizara ya Afya na iliyokabidhiwa Kamati ya Seneti kuhusu Afya, waziri alimwagiza Bi Ramadhani kukutana na mwanamume kwa jina Ken Ogola na “kumpa usaidizi wowote anaohitaji.”

“Bi Terry Ramadhani, anayekukabidhi kijibarua hiki Bw Ken Ogola ninamfahamu vyema. Mpe usaidizi anaohitaji,” kilisema kijibarua hicho.

Bi Ramadhani, hata hivyo, alieleza kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson Mandago, kwamba alitilia shaka agizo hilo la waziri na hakukutana na Bw Ogola.

“Waziri aliniarifu kuwa kuna kampuni ambayo ingepatia Kemsa vyandarua vya bure. Kwa sababu ninafahamu mchakato wa kuizawadi serikali, kukubali vyandarua bila malipo lilikuwa jambo la kutiliwa shaka mno,” alisema.

“Alizungumzia vilevile kuhusu ada fulani ya usajili ambapo nilimweleza Kemsa huwa haitozi ada yoyote.”

Aidha, afisa huyo aliyeachishwa kazi alielezea Kamati hiyo jinsi alivyoshtuka kufahamu kupitia vyombo vya habari kuhusu hatua ya waziri Nakhumicha ya kumsimamisha kazi.

Alisisitiza kuwa alifuata taratibu zote zinazohitajika kwenye mchakato wa kutoa zabuni ya Sh3.7 bilioni ya vyandarua kwa shirika la kimataifa la Global Fund na hakuelewa kilichosababisha zabuni hiyo kakataliwa.

“Hata mimi sijui kinachoendelea. Tulifuata taratibu zote zinazohitajika kwa sababu hiyo ni bidhaa yenye thamani kuu ambapo huwezi kuficha lolote. Ilikuwa muhimu kwetu kufuata masharti yote kikamilifu,” alisema.

Kulingana naye, sababu zilizotolewa na Global Fund kama misingi ya kufutilia mbali zabuni hiyo ya mabilioni hazikuwa na mashiko ikizingatiwa kwamba si mara ya kwanza kufanya kazi na shirika hilo.

“Baadhi ya sababu walizotoa ni kwamba nakala hazikuwasilishwa kwa pamoja na eti hazikuwa na nambari. Nilisema wazi mimi kama mkurugenzi sikuelewa sababu zao za kufutilia mbali zabuni. Hii haikuwa mara ya kwanza kutoa zabuni kwa Global Fund na muda wote huo hakujawahi kuwa na tatizo licha ya kuwasilisha nakala kando kando,” alisema Bi Ramadhani.

“Hatukuweza kufikia kiini kwa sababu wiki ambayo tulikuwa tumeandaa kikao cha kusuluhisha masuala hayo, ndipo tuliposimamishwa kazi.”

Bi Ramadhani alisema amebaki katika hali ya sintofahamu kwa sababu hajapokea mawasiliano yoyote rasmi tangu alipofahamishwa kuhusu hatua ya kumsimamisha kazi.

Sakata hiyo ya Kemsa imeonekana kuchukua mkondo mpya huku maafisa wakuu waliofutwa na kusimamishwa kazi wakililia haki.

Haya yamejiri wiki chache tu baada ya Rais William Ruto kumtimua Katibu wa Wizara ya Afya katika Idara ya Afya ya Umma, Dkt Josephine Mburu kuhusiana na mchakato wa zabuni ya Sh 3.7 bilioni kutoka shirika la kimataifa la Global Fund.

Aidha, Kiongozi wa Taifa alifutilia mbali teuzi za mwenyekiti na wanachama wa Bodi ya Kemsa hatua iliyotangazwa na Mkuu wa Watumishi wa Umma, Felix Koskei, kupitia taarifa mnamo Mei 15.

Hata hivyo, akijitetea mbele ya kamati hiyo vilevile, Dkt Mburu alijitenga na kashfa hiyo akisema hakuwa amechukua usukani ilipofanyika.

Kulingana naye, sakata hiyo ilitokea chini ya usimamizi wa aliyekuwa katibu wa Wizara ya Afya wakati huo, Peter Tum, ambaye sasa amehamishwa katika Wizara ya Masuala ya Vijana, Spoti na Sanaa.

Aidha, aliomba kusikiza upande wake akisema kuwa alifahamu kuhusu hatua ya kumfuta kazi kupitia vyombo vya habari.

“Nimekuwa mtumishi wa umma kitaaluma kwa miaka 34 bila kukumbwa na kesi yoyote. Hatua ya kunifuta kazi ilinipata ghafla. Sikuhusika kwa vyovyote na mchakato wa zabuni ya vyandarua vya mbu. Japo sitapinga uamuzi wa Rais lakini ningependa kujua alichoambiwa kilichomfanya kunitimua,” alisema Dkt Mburu.

  • Tags

You can share this post!

Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola sasa yagonga...

Macho yote kwa Spika Wetang’ula akitarajiwa kukabili...

T L