• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 6:24 PM
Samboja aendelea kuandamwa na kesi kuhusu cheti

Samboja aendelea kuandamwa na kesi kuhusu cheti

NA LUCY MKANYIKA

KESI inayopinga azma ya Gavana wa Taita Taveta, Granton Samboja kutetea kiti chake sasa itasikilizwa katika Mahakama ya Mombasa.

Kesi hiyo ambayo awali ilikuwa imewasilishwa katika Mahakama ya Nairobi na Bw Jeremiah Kiwoi, imehamishwa hadi jijini Mombasa ili isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa, Bi Njoki Mwangi, tayari ametenga Julai 6 ili kusikiliza kesi hiyo.

Jaji Mwangi aliagiza wahusika wote kupeana karatasi zote kuhusu kesi hiyo.

Katika ombi lake, Bw Kiwoi anataka mahakama itoe maagizo ya kuzuia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza Bw Samboja kuwa mgombeaji wa ugavana Taita Taveta hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa.

Mlalamishi huyo anapinga uhalali wa cheti cha shahada ya gavana huyo na kuomba afungiwe nje ya uchaguzi wa Agosti 9.

Anaitaka mahakama kumzuia Bw Samboja kuwania kwa kukosa kuzingatia masharti kuhusu uongozi na uadilifu.

Anasema gavana huyo alitumia njia za ulaghai kuidhinishwa 2017 alipodanganya kuwa alifuzu shahada ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Pia , mlalamishi anadai kuwa ni wazi kuwa shahada hiyo ni ya kughushi baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na chuo hicho kuthibitisha kuwa Bw Samboja hakuwa mwanafunzi katika taasisi hiyo.

Mnamo Juni, IEBC ilikuwa imemuidhinisha gavana huyo na kumpa nafasi ya kutetea kiti chake.

Bw Samboja anatetea kiti hicho kupitia chama cha Jubilee.

Mlalamishi anadai gavana huyo aliidhinishwa na IEBC baada ya kuwasilisha cheti cha digrii kutoka Chuo Kikuu cha Costa Rica. Lakini Bw Kiwoi alielekea mahakamani akidai vyeti vya Bw Samboja ni vya kutiliwa shaka.

Mlalamishi anasema IEBC inafaa kumzuia gavana huyo kutetea kiti chake kwani hana karatasi halali zinazohitajika ili kuidhinishwa na IEBC.

Mlalamishi anadai Bw Samboja hafai kuruhusiwa kuwania kiti hicho tena akitumia karatasi aliyotumia miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, ombi lake kwa mahakama hiyo lilitupiliwa mbali kwa msingi kwamba, Bw Samboja aliipatia IEBC cheti halali cha digrii.

Kufuatia uamuzi wa mahakama hiyo, Bw Kiwoi sasa amerudi mahakamani tena akilalamika kuwa mahakama hiyo ilifanya makosa kutupilia mbali ombi lake na huenda wakazi wa Taita Taveta wakachagua mtu asiyehitimu kwa kazi ya ugavana.

  • Tags

You can share this post!

Mtetezi aomba KWS ipewe ufadhili zaidi

Walioacha shule wakimbilia masomo ya uzeeni kujinusuru

T L