• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Seneta Sifuna amkashifu ‘Mtoto Wa Maumau’ Gachagua kwa kuagiza ‘sea food’ badala ya mutura

Seneta Sifuna amkashifu ‘Mtoto Wa Maumau’ Gachagua kwa kuagiza ‘sea food’ badala ya mutura

Na LABAAN SHABAAN

Seneta wa Nairobi Bw Edwin Sifuna amemshambulia Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua kwa kuagiza vyakula vya baharini (sea food) akisema haiendi sambamba na anavyojisawiri kama ‘jamaa wa mashambani’ kama anavyorejelea Bw Gachagua, huku akiteta kuwa itaongezea Wakenya gharama.

Bw Sifuna ameshangaa jinsi Bw Gachagua amevutiwa na maisha ya kula vyakula vya bahari, mito na maziwa kama vile samakikamba aina za molluscan, prawn na krestasia na vingine kama kaa (crab), Sulisuli (marlin), tuna na kambamti (lobster) akieleza kuwa “mtoto wa maumau” anafaa kuagiza mutura (chakula kinachouzwa mitaani na hutengenezwa kwa utumbo wa ng’ombe, mbuzi au kondoo ambamo damu, nyama na viungo hushonewa ndani kisha kuchomwa).

Aghalabu mlo wa baharini huliwa maeneo ya pwani na utavipata katika orodha ya vyakula kwenye hoteli za kifahari.

“Ofisi ya Naibu Rais ilitoa tangazo la zabuni ya sea food. Huyu ni mtu wa mutura. Gachagua anajua nini kuhusu vyakula vya bahari? Anatafuta sea food ya nini na ni kwa gharama ya pesa zetu za ushuru!” Bw Sifuna alifoka alipokuwa katika mjadala wa runinga ya Citizen Alhamisi asubuhi.

Seneta Sifuna amelalamika kwa kuongezeka kwa bajeti ya Ofisi ya Rais, Naibu wake na Mkuu wa Mawaziri kwa Sh3.4B mwaka wa fedha wa 2022/2023 akitaja kuwa fedha hizi zinatumika kwa sherehe na ziara za kila wakati.

Haya yanajiri siku kadhaa baada ya Naibu Rais kurejea nchini kutoka ziara za Colombia iliyodumu siku zisizopungua nne huku Rais William Ruto kufikia leo Septemba 21, 2023 akiwa angali ziara ndefu nchini Amerika.

“Mnafaa kupunguza gharama hii kwanza kabla ya kuwaambia Wakenya wakaze mishipi na inafaa serikali irejeshe ruzuku kupunguza gharama ya maisha,” Bw Sifuna akateta akiashiria serikali inaogopa kufuata mapendekezo yao kwa sababu upande wa upinzani utaonekana ulikuwa sahihi.

Seneta wa Nairobi amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kenya Kwanza katika majukwaa ya kisiasa na vyombo vya habari akidai serikali imeenda kinyume na manifesto ya kujali mahasla.

  • Tags

You can share this post!

Vibanda vya mahasla kujitafutia riziki vyabomolewa South B

Kayange: Shujaa wa 7s aliyewasha msisimko wa raga nchini na...

T L