• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Sheikh alalamikia kuitwa mchawi kufuatia mzozo wa mali ya Msikiti

Sheikh alalamikia kuitwa mchawi kufuatia mzozo wa mali ya Msikiti

Na TITUS OMINDE

SHEIKH mmoja kutoka Eldoret amelalamikia kuhusishwa na uchawi ili azuiwe kuhudhuria ibada ya msikiti.

Sheikh Diriwo Jamaal, aliambia mahakama kwamba viongozi wa kamati ya udhamini wa mskiti wa Jamia ndio wanasakata njama hiyo.

Sheikh huyo alidai kuwa hatua yake kutaka viongozi husika kuwajibikia mali ya msikiti huo, ndiyo ilifanya kamati hiyo kumbandika mchawi ili kumnyima uhuru wa kuabudu msikitini humo.

“Kamati ya msikiti wa Jamia ilikiuka haki zangu za kuabudu kwa kunitaja kama mchawi ili kunizuia kuingia msikitini na kushiriki ibada,” Diriwo aliambia mahakama.

Katibu wa kamati ya mskiti huo, Bw Chumo ambaye aliwasilisha hoja ya kupinga madai ya Bw Diriwo alikuwa na wakati mgumu kufafanua alichomaanisha kwa kumtaja Diriwo kama mchawi kupitia stakabadhi ambazo aliwasilisha mahakamani.

Kwenye stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, Chumo alimtaja Sheikh Diriwo kama mchawi ambaye anaamini ushirikina na hapaswi kujihusisha na uongozi wa shughuli za mskiti.

Bw Chumo alikuwa na wakati mgumu kushawishi mahakama kuhusu vigezo alivyotumia kubaini kuwa Bw Diriwo ni mchawi.

“Niliamua kumuita mchawi kutokana na tabia yake ya kujiita mganga ambaye anatibu uchawi. Sisi kama Waislamu tunaamini kuwa waganga ni wa wachawi,” Bw Chumo aliambia mahakama.

Hata hivyo, Bw Diriwo alipinga madai hayo huku akisema ilikuwa njama ya kumzuia kushiriki ibada na kuuliza maswali kuhusu mali ya mskiti.

Diriwo alisema hayo wakati wa kuuliza maswali katika kesi ambapo ameshtaki viongozi wa kamati ya msikiti kwa kujenga maduka  na kuendeleza biashara katika majengo ya mskiti, mbali na kudai kuwa kamati hiyo ni haramu.

Akijitetea dhidi ya tuhuma hizo kama katibu wa kamati ya mskiti huo Bw Chumo alipinga madai hayo huku akishikilia kuwa maduka hayo si kizingiti kwa shughuli za mskiti ikizingatiwa kuwa milango yake iko nje ya boma la mskiti.

“Mijengo hiyo haiko ndani ya msikiti lakini iko kwenye ukingo wa ua la msikiti. Maduka yameelekezwa nje ya msikiti,” aliiambia mahakama.

Alisisitiza kuwa Katiba iko wazi kuhusu suala hilo na kwamba kamati haijafeli kisheria kwa kuruhusu miundo hiyo kujengwa kwenye msikiti.

Uhalali wa ofisi ya sasa pia ulitiliwa shaka huku Diriwo akimshutumu shahidi huyo kuwa tapeli.

Kulingana na mlalamishi, Kamati ya Msikiti ya Muslim Association, Eldoret ilisajiliwa mwaka wa 2011.

Alibainisha kuwa wanaodaiwa kuwa viongozi wa kamati ya sasa walisajili chama tofauti, Muslim Association Mosque Committee baada ya kuwasilisha ombi lake.

“Hapana sio kweli, hili ni shirika moja,” Chumo alisema wakati wa mtihani huo.

Aidha, aliambia mahakama kuwa chama hicho kina viwanja 9 na akaunti moja ya benki ambayo ina mamilioni ya pesa.

Katika ombi lake, Diriwo anadai baadhi ya viwanja hivyo vimebadilishwa kinyume cha sheria na kuwa umiliki wa kibinafsi.

Bw Jamal alitaka mahakama iamuru ukaguzi wa mali zote za chama tangu 1990 huku akidai kuwa ripoti ya mwisho ya makabidhiano ilifanywa zaidi ya miaka 10 iliopita.

Mwishoni mwa waliojibu kuwasilisha shahidi wao, Jaji wa Mahakama Kuu ya Eldoret, Robert Wananda aliagiza pande zote kuwasilisha mawasilisho yao ya mwisho ndani ya siku 14.

Kesi hiyo itatajwa Julai 25, 2023, ili kutoa nafasi kwa mahakama kutoa uamuzi wake kuhusiana na kesi hiyo.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ligi ya Saudi Arabia itakuwa tano-bora karibuni –...

Mahakama yatupa kesi ya Itumbi kuomba CASs waruhusiwe...

T L