• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Simulizi ya mama yashtua mahakama

Simulizi ya mama yashtua mahakama

Na GEORGE MUNENE

Mama mmoja jana alisimulia mahakamani jinsi alivyopata chooni mifupa ya mwanawe na mjukuu wake ambao walikuwa wametoweka katika njia ya kutatanisha kwenye kijiji cha Uriro, Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.

Bi Pauline Kagendo na mwanawe Johnson Murithi ambaye alizaliwa miezi mitano iliyopita, walitoweka kwa njia ya kutatanisha mnamo Juni 10, 2017.

Mifupa hiyo ilipatikana ndani ya choo cha mpenziwe marehemu ambaye alikuwa afisa wa GSU.

Akitoa ushahidi mahakamani, mamake marehemu Kanini Nyaga alieleza Mahakama ya Embu kwamba mifupa hiyo iliyokuwa imeteketezwa ya mwanawe na mjukuu wakem ilipatikana ndani ya choo na makachero.

Mwanawe Bi Nyaga, alikuwa ameacha masomo katika kidato cha kwanza.Alikuwa akitoa ushahidi kwenye kesi ambapo afisa huyo wa GSU Edwin Mwenda alishtakiwa kwa kumuua Bi Kagendo na Bw Muriithi.

Bw Mwenda ambaye tayari ameachishwa kazi anawakilishwa na wakili Emies Mutegi na inadaiwa kuwa alikuwa mpenzi wa Bi Kagendo.

Bi Nyaga alidai kwamba mwanawe aliacha shule mnamo 2016 baada ya kupachikwa mimba na afisa huyo wa GSU ndipo akajifungua mtoto mvulana.

Alisimulia jinsi Bi Kagendo aliondoka nyumbani ili kumpeleka mwanawe hospitalini baada ya kuugua lakini hakurejea tena.

“Mwanangu alinieleza kwamba alikuwa anaenda kukutana na mpenziwe ili wote wawili wampeleke mtoto hospitalini kupokea matibabu lakini hakurejea nyumbani,” akaeleza mahakama alipokuwa akihojiwa na wakili David Njoroge.

Baada ya kumsaka mwanawe na mjukuu wake kwa muda wa mwezi moja, Bi Nyaga alipiga ripoti kuhusu kisa hicho katika kituo cha polisi cha Ishiara na uchunguzi ukaanza ndipo mifupa ya wawili hao ikapatikana kwenye choo ndani ya boma la Bw Mwenda.

You can share this post!

Saburi kusalia ODM wenzake wakihepa

Wito EACC ichunguze maafisa wa elimu