• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Sonko kuendelea kukaa hospitalini

Sonko kuendelea kukaa hospitalini

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ilielezwa jana kuwa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko angali amelazwa katika Nairobi Hospital anakopokea matibabu maalum.

Hakimu mkuu Bi Diana Mochache, wa mahakama ya kushughulikia kesi za ugaidi iliyoko Kahawa karibu na gereza kuu la Kamiti alielezwa na wakili Dkt John Khaminwa kwamba Sonko angali mgonjwa.

“Mheshimiwa Sonko hajapona. Hata unaona ameandamana na daktari kutoka Nairobi kuthibiti hali yake,” alisema Dkt Khaminwa.

Wakili huyo alisema Sonko anakabiliwa na changa moto kadhaa za kiafya na anahitaji kupokea matibabu kila mara.

Sonko alikuwa amefikishwa kortini mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DDP) awasilishe ombi la kumzuia Sonko kwa siku 30 kuhojiwa kwa madai anahusika na visa vya ugaidi.

Mahakama ilifahamishwa afisa anayechunguza kesi hiyo yuko safarini ng’ambo. Bi Mochache aliombwa aahirishe kesi hiyo kuwezesha mawakili wa Sonko kujibu ombi hilo azuiliwe kwa siku 30 kabla ya kuachiliwa.

Dkt Khaminwa aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo ndipo afisa huyo kutoka kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU) arudi kutoka ng’ambo.

Kesi hiyo itatajwa tena Feburuari 26,2020. Sonko alirudishwa Nairobi Hospital kuendelea na matibabu.

Mawakili hao waliomba muda wajibu madai ya ATPU kwamba Sonko amesajili kikosi cha wanamgambo ambao amewanunulia silaha na yunifomu kwa lengo la kuzusha vurugu nchini.

Lakini Bw Sonko amewashtaki DPP na Inspekta Jenerali (IG) akiomba wazimwe na mahakama kuu kumchunguza na hatimaye kumfungulia kesi za ugaidi akidai anadhulumiwa kisiasa.

Bw Sonko pia anaomba mahakama kuu iamuru aachiliwe mara moja kutoka kizuizini. Sonko anadai kuwa haki zake zimekandamizwa kufuatia kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

Gavana huyo anakabiliwa na kesi kadha za ufisadi na uvamizi wa ploti mtaani Buruburu. Pia ameshtakiwa kuwajeruhi watu sita wakati wa uvamizi huo wa 2019.

You can share this post!

Wambora ailaumu Serikali kwa kudhalilisha wakulima

Mnigeria akana kumlaghai raia wa Amerika Sh17 milioni