• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Tamaa ya visketi ilivyomponza Greenwood hadi akachujwa Man United

Tamaa ya visketi ilivyomponza Greenwood hadi akachujwa Man United

Na CHRIS ADUNGO

MUSTAKABALI wa fowadi Mason Greenwood kitaaluma sasa unazingirwa na wingu jeusi baada ya kuthibitishwa kwamba ataagana sasa na Manchester United kwa makubaliano baada ya uchunguzi wa miezi sita kuhusu mienendo yake kukamilika.

Greenwood, 21, alitiwa nguvuni mnamo Januari 2022 nje ya kasri lake lililoko Bowden-Cheshire, Uingereza, kufuatia kuchapishwa na kusambazwa mitandaoni kwa madai kadhaa dhidi yake.

Nyota huyo raia wa Uingereza alifunguliwa mashtaka, yakiwemo ya kujaribu kubaka na kushambulia mwanamke mmoja kwa nia ya kumdhibiti kwa nguvu na kumdhulumu kimapenzi. Alituhumiwa pia kumtishia maisha demu huyo na kutoa maoni ya kumdhalilisha kwenye mitandao ya kijamii kati ya Disemba 12-31, 2021.

Mashtaka hayo yote dhidi yake, ambayo yalitarajiwa kumpa kifungo cha maisha nchini Uingereza, yaliondolewa na mahakama mnamo Februari 2, 2023 baada ya mwathiriwa kukataa kushirikiana na maafisa wa upelelezi.

Baada ya kukamatwa, Man-United walimsimamisha kazi Greenwood kwa muda usiojulikana japo aliendelea kupokea mshahara wake wa Sh11.3 milioni kwa wiki. Mikataba ya mamilioni kati yake na kampuni za Nike na Electronic Arts pia ilikatizwa na jezi zote nambari 11 mgongoni alizokuwa akivalia kambini mwa Man-United zikaondolewa kwenye maduka ya mtandaoni ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Japo anahusishwa na uwezekano wa kuyoyomea Saudi Arabia, baadhi ya wadau wanahofia athari mbaya za kibiashara zitakazotokana na hatua ya kumsajili. Awali, ilikisiwa kuwa Greenwood angerejeshwa kambini mwa Man-United au kutumwa kwa mkopo katika kikosi cha Juventus, AC Milan, Inter Milan au AS Roma.

Sogora huyo sasa ni baba mzazi baada ya kipusa Harriet Robson kujifungua mtoto wao wa kwanza pamoja mwezi jana. Harriet, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Uingereza, alijifungua mnamo Julai 11, wiki mbili baada ya dume lake kufichua mpango wa kufunga naye pingu za maisha.

Alijiunga na Man-United akiwa na umri wa miaka sita pekee na akapanda ngazi hadi akapata nafasi ya kuvalia jezi za kikosi cha kwanza.

Mnamo 2019, aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuchezea Man-United katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) alipoingia ugani akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Amewajibikia Man-United mara 129 na kupachika wavuni mabao 35.

  • Tags

You can share this post!

Wafugaji ng’ombe wa maziwa Gatundu waelimishwa kuhusu...

Muuzaji mitishamba akamatwa kwa kuuza dawa zilizopigwa...

T L