WANAUME wengi kwenye vijiji vinavyoathiriwa na mashambulio ya Al-Shabaab kaunti ya Lamu wanaishi kwa hofu kufuatia hulka ya magaidi kuonekana kuilenga jinsia ya kiume wanaposhambulia.
Kati ya mwaka 2014 hadi sasa, Lamu imepoteza mamia ya wakazi mikononi mwa magaidi, ambapo karibu wote walioangamia ni wanaume.
Hali hiyo imewasukuma wanaume wengi kutolala majumbani mwao, ambapo wengine wameishia kutorokea kambini, kukodisha vyumba mijini au hata kulala misituni punde usiku unapowadia.
Wanaume wengi waliohojiwa na Taifa Leo kwenye vijiji husika walikiri kutokuwa na imani na usalama wa eneo hilo, ikizingatiwa kuwa wameshuhudia wenzao wengi wakiuawa kinyama na Al-Shabaab bila usaidizi wa walinda usalama.
“Utapata uvamizi wa kwanza ulioshuhudiwa pale mjini Mpeketoni, watu karibu 90 waliuawa usiku mmoja na wote walikuwa wanaume. Vile vile ukiangalia kwenye vijiji vyetu, magaidi wamekuwa wakiburuta wanaume pekee kutoka kwa nyumba zao kila wanaposhambulia na kuwachinja kama kuku ilhali wakilazimisha wanawake na watoto kutazama madhila hayo.
“Tuko na wasiwasi kama wanaume kuendelea kuishi na kulala ndani ya nyumba zetu hasa usiku,” akasema Bw Shadrack Njuguna, mkazi wa kijiji cha Juhudi ambaye ni mkimbizi kwenye kambi ya Juhudi Primary.
Sababu nyingine inayoashiria jinsi magaidi wanavyotafuta kwa udi na uvumba kuua wanaume kwenye vijiji vya Lamu ni wakati ambapo wanavamia maboma ya watu na kisha kupata ni wanawake na watoto pekee walioko.
Magaidi wamekuwa wakiwapa kisomo na mahubiri wanawake hao huku wakionya jinsi watakavyoendelea kuwalenga na kuwaua wanaume wao hadi pale serikali ya Kenya itakapokoma kutesa na kuua wenzao katika nchi jirani ya Somalia.
Jumatano wiki hii, Bi Eunice Mong’are, mkazi wa Widho-Mashambani alipatikana nyumbani na magaidi usiku akilala na wanawe watatu.
“Waliniuliza aliko mume wangu. Walipomkosa waliniachia ujumbe kwamba hawatachoka kuwatafuta waume wetu na kuwachinja ili kulipiza kisasi mauaji ambayo Kenya inatekeleza dhidi ya watu wao Somalia. Waliiba mahindi, unga, mbuzi na kuku na kisha kumuua shemeji yangu. Mimi na watoto hawakutugusa,” akasema Bi Mong’are.
Kulingana na Mwanasaikolojia, Bw Andrew Masama, magaidi wanaua wanaume kama njia mojawapo ya kuilemaza familia na jamii kwa jumla.
Pia ni njia mojawapo ya kuweka woga kwa jamii, hivyo kuwawezesha kutimiza ajenda zao, ikiwemo kuendeleza upotofu wa jamii na kusajili vijana kuingia kwenye kundi lao la kigaidi.
“Kimsingi, mwanamume katika familia ni kiungo muhimu. Yeye ni mlinzi, ni mwenye kuikimu familia na kuendeleza kizazi. Wanapomuua mwanamume inamaanisha familia hiyo haina kiongozi.
“Inalemaa na kusambaratika kabisa. Hapo utapata kama ni watoto wakikua kwa uoga. Wanapatwa na msongo wa mawazo mapema, hivyo wengine kuishia kujiingiza kwenye mambo potofu kama vile dawa za kulevya.
“Wakifanya hivyo inakuwa rahisi kwa Al-Shabaab kuwashawishi na kuwasajili kujiunga na kundi lao la kigaidi,” akasema Bw Masama.
Wakazi aidha waliisihi serikali kuzidisha nguvu vita dhidi ya Al-Shabaab eneo hilo.
Katibu wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Athman, aliwasihi wananchi, viongozi na serikali kwa jumla kutoingiza siasa suala la usalama eneo hilo na badala yake waungane kupiga vita uhalifu.