• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Ukiukaji wa haki za Miguna hatari kwa nchi – Mutunga

Ukiukaji wa haki za Miguna hatari kwa nchi – Mutunga

Na BENSON MATHEKA

UJASIRI wa Serikali ya Kenya wa kupuuza, kudharau na kukiuka maagizo ya mahakama unafaa kutia wasiwasi raia wa nchi hii wasukume maafisa wa serikali kuheshimu Katiba na utawala wa sheria, aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga ameonya.

Dkt Mutunga amesema kwamba hatua ya serikali ya kumzuia wakili anayeishi Canada Miguna Miguna kusafiri hadi Kenya, inafaa kuwatia wasiwasi raia wote wa Kenya na kuwataka viongozi waheshimu katiba waliyoapa kulinda.

Dkt Miguna alipaswa kuwasili Kenya Jumanne asubuhi lakini kampuni ya ndege ya Ufaranza aliyopaswa kutumia kusafiri ilikataa kumbeba kufuatia onyo kutoka kwa serikali ya Kenya.

Hatua hiyo ilijiri siku tatu tu baada ya serikali kuambia mahakama kwamba haikuwa imetoa onyo kwa safari za ndege kutombeba Bw Miguna Miguna au raia yeyote wa Kenya anayerejea nchini akiwa na stakaabadhi halali.

Jumanne, Dkt Mutunga aliungana na chama cha wanasheria nchini na wanaharakati kukashifu serikali kwa kuendelea kumnyima Bw Miguna haki zake za kikatiba ikijua wazi kuwa akiwa mzaliwa wa Kenya, uraia wake hauwezi kufutwa.

“Hatutalegeza juhudi zetu za kuhakikisha kwamba utawala wa sheria unaheshimiwa, haki za kila Mkenya zimelindwa na kuheshimiwa na kwamba mahakama zimeheshimiwa,” alisema Dkt Mutunga.

Alisema kwamba kati ya mihimili mitatu ya serikali ni mahakama pekee na mawakili wanaotetea haki za raia dhidi ya dhuluma za maafisa wa serikali.

“Serikali Kuu na Bunge hazijali maslahi ya raia, mwokozi wetu kwa wakati huu ni mahakama,” alisema.

Dkt Miguna alikashifu serikali kwa kuhadaa mahakama kwamba haikuwa imetoa onyo kwa kampuni za safari za ndege kutombeba Bw Miguna.

“Wiki jana, tulizungumzia suala la Bw Miguna na wiki jana, mahakama iliambiwa hakukuwa na onyo lolote. Lakini jana Jumanne, walifanya hivyo na kutuma onyo jingine. Tutafanya kila liwezalo kuhakikisha Miguna anarudi Kenya,” alisema na kuongeza kuwa walipotangaza kuwa Bw Miguna angerudi Kenya, walijua ingekuwa vigumu.

Akizungumza katika ofisi za chama cha United Green Movement Party, Dkt Mutunga alitaja onyo la serikali kwa kampuni za safari za ndege kutombeba Bw Miguna kama haramu kwa kuwa kuna agizo la korti kumruhusu wakili huyo kurudi Kenya.

Rais wa chama cha mawakili (LSK) alisema Wakenya wanafaa kuwa na hofu na kukasirishwa na hatua ya serikali ya kupuuza maagizo ya mahakama.

“Wanasiasa wamekuwa wakifanya mikutano ya kampeni na kutoa ahadi za kila aina lakini hakuna anayeahidi kuheshimu haki za raia na kulinda katiba. Hii inafaa kutupatia wasiwasi,” alisema.

Alisema kwamba wamewasilisha kesi kortini kwa lengo la kutaka serikali kuondoa onyo la kumzuia Bw Miguna Miguna kurudi Kenya.

You can share this post!

Shujaa yatiwa kundi moja na Amerika ya Mike duru ya Dubai...

Ugaidi: 6 wafa, 33 wakiumia Uganda

T L