• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Viongozi kutoka Kisii wadai Ruto huenda jimbo lao kuhubiri alivyoshinda Raila badala ya kupeleka maendeleo

Viongozi kutoka Kisii wadai Ruto huenda jimbo lao kuhubiri alivyoshinda Raila badala ya kupeleka maendeleo

NA SAMMY WAWERU

BAADHI ya viongozi wa jamii ya Abagusii wamemlaumu Rais William Ruto wakidai hutembelea jimbo lao kwa lengo la kujisifia jinsi alivyomshinda kiongozi wa upinzani, Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na viongozi hao, tangu Rais Ruto achukue mikoba ya uongozi Septemba 2022, hajatekeleza miradi yoyote ile ya maendeleo eneo la Kisii.

Chini ya Baraza la Omogusii katika Kaunti ya Nairobi, linamlaumu kiongozi wa nchi kwa kutembelea eneo hilo kwa lengo la kudunisha kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw Odinga.

“Ni nini amefanya katika eneo letu? Hakuna kitu kabisa. Anatembelea Jimbo la Kisii kumdhalilisha kiongozi wetu, Mheshimiwa Raila Odinga, kuhusu jinsi alivyomshinda mwaka wa 2022,” alisema Mwenyekiti wa kundi hilo, Joseph Nyandika akihutubia vyombo vya habari majuzi jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa Baraza la Omogusii katika Kaunti ya Nairobi, Bw Joseph Nyandika akihutubu. PICHA|SAMMY WAWERU

Baraza la Omogusii ni kundi linalowaleta pamoja wakazi wote wa jamii ya Kisii katika Kaunti ya Nairobi.

Lengo kuu la baraza hilo ni kukuza na kutimiza maslahi ya Abagusii jijini Nairobi.

Likipongeza utendakazi wa serikali za ugatuzi eneo la Kisii, kundi hilo lilisisitiza kuwa serikali ya Dkt Ruto haiwezi ikajivunia mradi wowote ule iliyozindua katika jimbo hilo.

Aidha, eneo hilo linajumuisha Kaunti za Kisii na Nyamira.

“Waziri Mkuu wa zamani (akimrejelea Bw Raila Odinga) amekuwa amesimama kidete nasi. Tumekuwa na wawakilishi katika serikali (serikali za nyuma) anazohusishwa nazo. Jamii ya Abagusii inanyanyaswa na serikali ya sasa,” alidai Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw Benson Omae.

Baadhi ya viongozi wawakilishi wa Baraza la Omogusii Nairobi wakisalimiana baada ya kufanya kikao na wanahabari katika Jengo la Bomblast, Jijini Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Kundi hilo lilipongeza Bw Raila ambaye pia ni kiongozi wa mrengo wa Azimio la Umoja – One Kenya kwa kile walichosema “amejitolea kuhakikisha jamii zilizonyimwa haki zina sauti katika chama chake”.

Viongozi hao, kwenye kikao na vyombo vya habari katika Jengo la Bomblast, Jijini Nairobi, walitaja uchaguzi wa Madiwani (MCAs) 5 jijini Nairobi chini ya chama cha ODM, mmoja aliyeteuliwa kujiunga na bunge la jiji (Bi Naomi Bosire), na aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Kaskazini awali, Bw Simba Arati (ambaye kwa sasa Gavana wa Kaunti ya Kisii), kama baadhi ya ahadi za Bw Raila Odinga ambazo zimefanya eneo la Abagusii kuwa ngome ya upinzani.

“Sisi kama Baraza la Omogusii Nairobi, tuna kila sababu ya kusimama kidete na kuunga mkono Raila Odinga. Ametufanyia makubwa kama jamii, na tunaomba kudumisha nafasi ya awali ya Katibu Mkuu wa Chama cha ODM, Kaunti ya Nairobi,” Bw Nyandika alisisitiza.

  • Tags

You can share this post!

Harambee Stars yalenga kujinyanyua leo dhidi ya Ushelisheli

Bei za mafuta, umeme kupanda tena mswada mpya ukipitishwa

T L