NA SAMMY KIMATU
WAFANYABIASHARA waliokuwa wamebomoa nyumba na vibanda vya kibiashara kupisha mradi wa ujenzi wa barabara ulioanzishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta eneo la South B, kaunti ndogo ya Starehe wamevamia pande mbili za barabara na kuanza kujenga upya vibanda, mhandisi amelalamika.
Lakini waliohojiwa wamedai kwamba barabara hiyo ya umbali wa nusu kilomita inajengwa polepole na wanakandarasi wawili waliopewa kazi hiyo.
Mnamo Jumatatu, wafanyabiashara hao walikuwa na shughuli nyingi wakiwahudumia wateja wao katika sehemu ya barabara ya Hazina-Kayaba.
Katika mtaa wa mabanda wa Hazina, vibanda vilivyojengwa kwa mabati vimejengwa vikiegemea ua unaozunguka mtaa wa Hazina.
Mhandisi ambaye alikataa kutajwa jina na waandishi wa habari, alisema eneo hilo limetengwa kwa ajili ya uchimbaji wa mtaro wa kusafirisha maji machafu, milingoti ya taa na njia ya wanaotembea kwa miguu.
“Tukirudi kuanza kazi tena, tutabomoa vibanda vyote vilivyojengwa katika sehemu hiyo iliyoratibiwa kufanyiwa kazi ya njia ya watu kutumia, taa za barabara na mtaro wa majitaka,” mhandisi huyo mwanamume akasema.
Baadhi ya waliozungumza na Taifa Leo walisema wanakadiria hasara baada ya kubomoa nyumba zao na vibanda vya biashara wakisema ujenzi wa barabara hiyo yenye umbali wa nusu kilomita haujakamilika tangu ulipozinduliwa miaka mitatu iliyopita.
“Huu ni mzaha. Barabara hiyo ilipangwa kukamilika ifikapo 2021 lakini wanakandarasi wawili waliacha kufanya kazi. Uchumi ni mbaya na unatuumiza. Ni lazima tufanye kazi ili kulisha familia zetu na kusomesha watoto,” mama ambaye huuza samaki alisema.