• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Wafuasi wa Maina Njenga wazushia DCI

Wafuasi wa Maina Njenga wazushia DCI

NA STEVE OTIENO

RABSHA zilizuka katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) baada ya kiongozi wa zamani wa Mungiki Maina Njenga kufika huko kuhojiwa.

Hii ni baada ya mamia ya wafuasi wake kutaka kuingia katika afisi hizo kwa nguvu kushikiniza kuachiliwa kwa mwanasiasa huyo.

Bw Njenga alikuwa ameagizwa kufika katika makao hayo makuu ya DCI yaliyoko barabara ya Kiambu Road baada ya maafisa wa polisi wa Nakuru kudai walipata bunduki mbili na zaidi ya misokoto 90 ya bangi katika makazi yanayohusishwa na mwanasiasa huyo katika eneo la Ngomongo, kaunti ndogo ya Bahati.

Polisi walilazimika kurusha vitoa machozi kuwatawanya watu hao, wengine wao wakiwa vijana, waliotaka kuingia katika afisi za DCI wamkomboe Bw Njenga.

Purukushani hizo zilitatiza mwendo wa magari katika barabara hiyo. Hatimaye polisi walifaulu kuwatawanya vijana hao walioelekea barabara kuu ya Thika.

Kundi la viongozi wa Azimio wakiwemo kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, kiongozi wa chama cha Roots George Wajackoyah, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria pia walienda katika afisi hizo za DCI kumtetea Bw Njenga.

Hata hivyo, viongozi wa Azimio wanasema kuwa masaibu ya Bw Njenga yamechochewa kisiasa.

Walimsuta Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kwa kuwatumia polisi kuendesha vita vya kisiasa dhidi ya wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Azimio.

Viongozi hao wa Azimio walisema kuamriwa kwa Bw Njenga afike kwa DCI kulikuwa na njama kuhujumu wanasiasa kutoka Mlima Kenya wanaopinga utawala wa Kenya.

Bw Kioni aliongeza kuwa kuandamwa na Bw Njenga pia ni hatua ya kuwatisha wafuasi wa Azimio kutoka Mlima Kenya ili wajiunge na Kenya Kwanza akisema hiyo ni kinyume cha Katiba.

“Kenya Kwanza wanadharau uhuru wa kikatiba wa wenzetu kutoka Mlima Kenya kujihusisha na shughuli za Azimio. Ningependa kuwaambia kuwa hatutatishika,” akasema.

Bw Kioni alikosoa jinsi serikali ilishughulikia kesi ya Bw Njenga akisema polisi waliwahadaa kisha wakamtorosha “mteja wangu na kumpeleka kusikojulikana.”

“Tulikuwa zaidi ya mawakili sita tuliofika DCI kumwakilisha Bw Njenga. Tulipokuwa tukishauriana na mteja wetu polisi waliomba tumruhusu akamilishe jambo fulani. Punde tu Bw Njenga alipoondoka, polisi walimfungia katika chumba tofauti bila kutuarifu. Hii ni kinyume cha sheria,” Bw Kioni, ambaye ni Mbunge wa zamani wa Ndaragua, akasema.

Bw Kioni alisema utawala wa Kenya Kwanza unajizatiti kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya haliungani na kuongea kwa sauti moja kisiasa.

Hii, akasema, ni kwa sababu muungano huo tawala umeng’amua kuwa umeanza kupoteza umaarufu katika eneo la Mlima Kenya baada ya kufeli kutimiza ahadi nyingi ulizotoa kwa wakazi.

  • Tags

You can share this post!

Ikulu kukosa stima siku nzima – Kenya Power

Wakazi wa Keiyo wakataa naibu chifu asiye mwenyeji

T L