• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Wahalifu watumia maombi kuwahadaa wakazi wa Thika

Wahalifu watumia maombi kuwahadaa wakazi wa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WASHUKIWA wanane wa ulaghai wanaojidai wana uwezo wa kuombea watu na ‘kuongeza pesa’ wamevamia mji wa Thika.

Mnamo Jumamosi washukiwa hao walimhadaa mwanamke mmoja mjini Thika huku wakidai kuwa wangemuombea ili pesa zake ziongezeke maradufu.

Kwa siku chache zilizopita wakazi wengi wa Thika wamepoteza pesa zao na mali kupitia walaghai hao.

Jambo la kwanza wanalofanya ni kumsalimia mhusika kwa mkono na mwathiriwa anapokubali huwa wameshamnasa tayari.

Mwanamke mmoja aliingia katika mtego huo baada ya kutakiwa apige magoti ili aombewe pesa zake ziongezeke maradufu.

Baada ya mwanamke huyo kukubali maagizo yao alifumba macho huku akitarajia kuombewa ili apate pesa nyingi.

Kufumba na kufumbua mama huyo alijipata akiwa pekee yake huku washukiwa hao wakiwa wametoweka.

Hata hivyo, alipiga mayoe huku wananchi wakiingilia kati ili kumsaidia.

Katika hali hiyo washukiwa wengine saba walitoweka huku mmoja akinaswa na umati.

Mshukiwa huyo mmoja alipelekwa kituo cha polisi cha Thika baada ya kutambuliwa na mwanamke huyo aliyepoteza pesa zake na kibeti.

Kamanda mkuu wa Polisi wa Thika, Bi Beatrice Kiraguri, alithibitisha kisa hicho na kusema mshtakiwa atahojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani Jumatatu ili kujibu mashtaka ya ulaghai na wizi.

Afisa huyo wa polisi alisema polisi wataendelea kuweka doria saa 24 katika mji huo na vitongoji vyake ili kukabiliana na hali hiyo.

Kwa muda wa wiki chache zilizopita kumekuwa na wizi wa vibeti unaoendeshwa na vijana wadogo mjini Thika.

Wakazi kadha wa mji wa Thika na maeneo ya karibu wamefurahia hatua hiyo ya kuweka polisi katika maeneo yao kukabiliana na wahalifu hao.

Wahalifu hao huendesha wizi wao majira ya asubuhi wakati watu wakielekea kazini na jioni wanaporejea nyumbani.

You can share this post!

Yaya aliyewajeruhi watoto wa mwajiri aliyemfuta kazi atiwa...

SHAIRI: Ubakaji kama makaa