• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Wakazi wa Mombasa wafurahia daraja jipya la kuelea Liwatoni

Wakazi wa Mombasa wafurahia daraja jipya la kuelea Liwatoni

Na DIANA MUTHEU

WAKAZI wa Mombasa wana raha baada ya serikali kuwaruhusu kutumia daraja jipya la kuelea la Liwatoni kuvuka kutoka kisiwa cha Mombasa hadi upande wa Likoni, siku ya Krismasi.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali, wakazi hao walisema kuwa mradi huo utasaidia kupunguza msongamano katika kivuko cha feri cha Likoni, na kuwazuia dhidi ya kuambukizana naradhi ya Covid-19.

Walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja hadi mwingine, wakazi wengi walisema kuwa walihisi wako salama wakitumia daraja hilo.

“Mwanzo nilidhani kuwa daraja hili lingekuwa linaning’inia hewani, lakini nimeliona, nikavuka, na kwa ukweli nimejihisi nikiwa salama kabisa,” akasema mkazi mmoja, Bi Jecinta Jepkoech akisema kuwa hatahitaji kusubiri feri ndipo aweze kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Akizungumza katika daraja hilo, mshirikishi wa eneo la Pwani, Bw John Elungata alisema kuwa daraja hilo lilitengenezwa rasmi ili kupunguza msongamano katika kivuko cha feri cha Likoni.

Alisema kuwa katika daraja hilo, wakazi wanaweza kufuata sheria za kukaa umbali wa mita moja unusu wanapovuka.

Lakini wakazi waliruhusiwa kutumia daraja hilo kuanzia saa nne hadi saa nane tu.

“Wananchi wataanza kutumia daraja hili rasmi mnamo Desemba 31,” akasema Bw Elungata huku akiwahakikishia wakazi kuwa usalama utadumishwa katika daraja hilo.

“Daraja litakapoanza kutumiwa rasmi, wakazi wataweza kuvuka kuanzia saa kumi asubuhi hadi saa mbili jioni, lakini litakuwa linafunguliwa kupisha meli,” akasema.

Zaidi, Bw Elungata alisema kuwa hawataruhusu magari, pikipiki na tuktuk kutumia daraja hilo.

Kaimu Mkurugenzi Msimamizi wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA), Bw Rashid Salim alisema kuwa idara ya kushughulikia maswala ya majini ilikuwa imeelezewa kuhusu hafla yao, na zaidi watatangaza mikakati kabambe kuhusu matumizi ya daraja hilo, wakiendelea kuliimarisha .

You can share this post!

Shoo ya #WifeMaterial yamtia Eric Omondi matatani

SHAIRI: Msirarue maisha yangu