• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Wakulima Homa Bay wasusia mbolea ya bei nafuu

Wakulima Homa Bay wasusia mbolea ya bei nafuu

NA GEORGE ODIWUOR

HUKU serikali ikijiandaa kusambaza mbolea ya bei nafuu kwa wakulima wasiopungua 500,000 katika Kaunti ya Homa Bay imebainika baadhi ya wakulima wanaisusia.

Mbolea hiyo itakayosambazwa kupitia vituo mbalimbali inadhamiriwa kuongeza uzalishaji chakula katika eneo la ziwani.

Hata hivyo, sio wakulima wote wanaotumia mbolea wakati wa upanzi kutokana na imani kuwa huwa inapunguza mazao.

Kamishna wa Kaunti Moses Lilan alisema wakulima wasiopungua 150,000 waliandikishwa mnamo Machi kabla ya msimu wa upanzi mwaka huu Aprili.

“Sasa tunataka kuongeza idadi ifike 500,000. Haya yatafanyika katika awamu ya pili ya usajili,” alisema Bw Lilan.

Katibu wa Chama cha Ushirika kuhusu Thamani ya Pamba Kaunti ya Homa Bay Apiyo Oloo, alisema baadhi ya wakulima wanaamini udongo wa kaunti hiyo una rutuba ya kutosha kustawisha uzalishaji chakula.

Chama hicho cha ushirika kina wanachama 7,610.

Bw Oloo alisema hakumbuki akiona mwanachama wake yeyote akiendea mbolea hiyo mwezi Machi.

“Hakuna mkulima yoyote aliyetumia mbolea kupanda pamba katika misimu iliyopita. Kuna Imani kwamba udongo una rutuba ya kutosha kufanikisha kilimo cha mimea,” akasema.

Serikali kuu na ile ya kaunti zinashirikiana kusajili wakulima. Wakulima wa mimea mingine nao wana wasiwasi kuhusu aina ya mbolea ambayo watapokea.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Lolwe Karachuonyo Ager Kirowo alitaka serikali itathmini kwanza aina ya udongo katika eneo hilo kabla ya kuanza kusambaza mbolea.

Anasema kuna baadhi ya wakulima waliofanyiwa ukaguzi wa mchanga na kushauriwa kutumia aina fulani ya mbolea.

“Ikiwa shamba lina mchanga wenye asidi, mkulima anafaa kuchukua mbolea ya chachu. Hata hivyo, serikali ilisambaza mbolea aina moja bila ya kutilia maanani jambo hili la udongo,” akasema Bw Kirowo.

  • Tags

You can share this post!

Demu alia kukosa ‘nyota’ ya kupata dume la...

Wana walioadhibiwa ODM warudi Ikulu kupata mawaidha ya Rais...

T L