• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Walanguzi wa dawa za kulevya wasukumwa jela kula maharagwe

Walanguzi wa dawa za kulevya wasukumwa jela kula maharagwe

NA RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Tanzania amefungwa miaka 20 bila faini kwa ulanguzi wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh11 milioni.

Nassoro Salim Said alipatikana na hatia ya ulanguzi wa gramu 3, 921.6 za heroini katika eneo la Mlolongo, Kaunti ya Machakos.

Said anayeishi mtaa wa Balozi, jijini Dar-es-Salaam alihukumiwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Bernard Ochoi.

Wakati huo huo, Bw Ochoi alimhukumu Elizabeth Njoki Wanjiru aliyeshtakiwa pamoja na Said kifungo cha miaka mitatu bila faini kwa kupatikana amehifadhi gramu 1, 314.9 za heroini katika makazi yake mtaani Umoja III Septemba 2, 2016.

Wote wawili; Said na Njoki walikamatwa katika eneo la Mlolongo.

Akipitisha hukumu, Bw Ochoi alisema upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya washtakiwa hao.

“Hii mahakama inatilia maanani kwamba dawa za kulevya zimeathiri familia nyingi kote ulimwenguni na wanaonadi mihadarati wanapasa kuadhibiwa vikali,” alisema Bw Ochoi katika hukumu yake.

Hakimu aliendelea kusema, wanaouza dawa za kulevya ni adui kwa jamii na “kamwe hawapaswi kuonewa huruma.”

Bw Said hakufika kortini ila hakimu aliamuru akamatwe na kupelekwa jela.

Said alikamatwa akisafirisha dawa hizo kwa kutumia gari lenye nambari za usajili wa Tanzania T321 CVY, Toyota Prado rangi nyeusi.

Mahakama iliamuru polisi wa humu nchini wawasiliane na polisi wa kimataifa almaarufu Interpol kumtia nguvuni Said na kumrejesha nchini atumikie kifungo.

“Kifungo cha Said kitaanza kutumika pindi atakapotiwa nguvuni,” aliamuru Bw Ochoi.

Njoki alijitetea akisema ni mama mwenye watoto wawili wanaomtegemea.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka aliomba kosa la Njoki lichukuliwe kuwa la kwanza.

Bw Ochoi alimpa Njoki siku 14 kukata rufaa.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya wa miaka 52 ashtakiwa Amerika kwa kupanga kuua bibi...

Watumiaji TikTok kuanza kuchuma hela na zawadi

T L