• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Waliokamatwa kwenye msako mkali Mukuru kufikishwa kortini Alhamisi

Waliokamatwa kwenye msako mkali Mukuru kufikishwa kortini Alhamisi

NA SAMMY KIMATU

WASHUKIWA 37 wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mnamo Alhamisi baada ya kukamatwa kwenye msako mkali wa polisi ulioendeshwa katika maeneo matatu ya Mukuru usiku wa kuamkia leo Jumatano.

Naibu kamanda wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Collins Omuko amesema katika msako wa kwanza, watu 10 walikamatwa. Operesheni ililenga wahalifu sugu wanaoshika watu kabari usiku katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Reuben.

“Katika kundi la pili, msako uliondeshwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Makongeni uliwanasa washukiwa 17 wakiwemo washikaji kabari, wachezaji kamari, wenye baa zisizo na leseni miongoni mwa makosa mengine,” Bw Omuko akawaambia wanahabari.

Vilevile, katika msako wa tatu ulioendeshwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Industrial Area, maafisa hao wamekamata washukiwa 10.

Baadhi ya washukiwa walikuwa na makosa ya kufungua vilabu bila leseni huku wengine wakikamatwa kwa kubugia pombe haramu ya chang’aa na wengine wakipatikana wakiwa walevi waliokosa adabu.

“Lengo la misako yote ni kuhakikisha sheria inafuatwa na walio kwenye biashara ya pombe. Vilevile ni vizuri nao wananchi wajue kuna saa serikali imepatiana za kunywa pombe na saa za vilabu kuhudumu na kutohudumu. Polisi hawana nia mbaya ya kuwadhulumu wananchi wetu ila ni kazi inayofanywa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu,” Bw Omuko akafafanua.

Kadhalika, Bw Omuko amewatahadharisha wale ambao huuzia watoto vileo na mihadarati.

Aidha amedokeza kwamba washukiwa wengine hasa wauzaji wa pombe haramu, hutumia nyumba zao kuwa maficho ya wahalifu na kuonya chuma chao ki motoni.

Mnamo Jumanne polisi wa kituo cha South B waliendesha msako mwingine uliofanyika kwenye mitaa ya mabanda ya Hazina na Maasai Village.

Katika operesheni hiyo, watu saba walikamatawa na mashine mbili za kuchezea kamari kutwaliwa.

Eneo la polisi la Makadara limeundwa kutokana na vituo vitano vya polisi na kambi zaidi ya tano pia za polisi.

Aidha, vituo hivyo ni pamoja na Makongeni, Industrial Area, South B, Reuben na Viwandani.

Awali, Bw Omuko alikiri kwamba viwango vya uhalifu vilikuwa juu kutokana na msongamano wa mitaa mingi ya Mukuru iliopo.

Hata hivyo, leo viwango vya usalama vimeenda chini kufuatia kuzinduliwa kwa vituo vinne zaidi baada ya kituo cha zamani cha Industrial Area.

“Nasema usalama umaeimarika maradufu kufuatia Mpango wa Nyumba Kumi na uhusiano mwema wa raia na Polisi. Pia ongezeko la maafisa wanaoshika doria saa 24 na uwepo wa kambi zetu karibu na makazi ya mitaa pamoja na magari tuliyopewa ya kuhudumia wananchi ni mambo yaliyochagia kupiga jeki usalama kaunti ndogo ya Makadara,” Bw Omuko asema.

  • Tags

You can share this post!

Richie Spice kutumbuiza na kula ngege Kisumu

Thamani ya Saka yapanda mara 5, sasa kutia mfukoni Sh2.5...

T L